Michezo

Kocha mpya wa Stars ataja kikosi cha wachezaji 21

May 13th, 2018 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

KOCHA mpya wa timu ya taifa ya soka ya Kenya, Sebastien Migne ametaja kikosi cha wachezaji 21 kwa kambi ya mazoezi ya siku moja kujinoa kwa mechi za kimataifa zijazo.

Kambi hii, ambayo itaandaliwa Mei 15 uwanjani Camp Toyoyo jijini Nairobi, inalenga kuwaangalia kwa karibu wachezaji hawa, ambao 20 wanasakata soka humu nchini.

Migne na kocha msaidizi Nicolas Bourriquet watakuwa na vipindi viwili vya mazoezi siku hiyo. Kipindi cha kwanza kitaanza saa mbili asubuhi na kumalizika saa tano asubuhi. Kipindi cha pili kimeratibiwa kufanyika kutoka saa kumi jioni hadi saa kumi na mbili jioni.

Beki wa Eric ‘Marcelo’ Ouma kutoka klabu ya KF Tirana nchini Albania ni mchezaji pekee anayetandaza soka ya malipo nje ya Kenya aliyejumuisha katika kambi hii.

Mchezaji huyu wa zamani wa Gor Mahia alitarajiwa kusakata mechi yake ya mwisho ya Ligi ya Daraja ya Pili ya Albania dhidi ya Bylis hapo Mei 12, 2018 kabla ya kufunga safari ya kuja Nairobi.

Katika hafla ya kutambulisha benchi mpya la kiufundi la Stars jijini Nairobi hapo Mei 3, Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) lilisema linatafutia timu hii angaa mechi mbili za kirafiki. Bado timu hizo hazijatangazwa. Mechi hizo zinatarajiwa mwisho wa mwezi huu wa Mei na mapema Juni.

Kikosi cha Harambee Stars:

Makipa

John Oyemba (Kariobangi Sharks), Timothy Odhiambo (Ulinzi Stars) na Patrick Matasi (Posta Rangers);

Mabeki

Yusuf Mainge (AFC Leopards), Bolton Omwenga (Kariobangi Sharks), David Owino (Mathare United), Dennis Sikhayi (AFC Leopards), Michael Kibwage (AFC Leopards), Jockins Atudo (Posta Rangers), Johnstone Omurwa (Mathare United), Geoffrey Shiveka (Kariobangi Sharks), Moses Mudavadi (St Anthony Kitale), Musa Mohamed (hana klabu) na Eric Ouma (KF Tirana, Albania);

Viungo

Chrispin Oduor (Mathare United), Vincent Wasambo (Kariobangi Sharks), Cliff Nyakeya (Mathare United), Patillah Omotto (Kariobangi Sharks), Duncan Otieno (AFC Leopards) na Marvin Omondi (AFC Leopards);

Washambuliaji

Elvis Rupia (Nzoia Sugar), Pistone Mutamba (Wazito) na Ovella Ochieng’ (Kariobangi Sharks).