Michezo

Kocha Odera ataja chipukizi wa Chipu tayari kuwinda tiketi ya JWRT

April 2nd, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

WENYEJI Kenya wametaja kikosi kitakachowania tiketi ya kushiriki mashindano ya dunia ya Junior World Rugby Trophy (JWRT) katika kombe la raga ya wachezaji 15 kila upande ya chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20 la Afrika almaarufu Barthes Trophy.

Kocha Paul Odera na vijana wake wa Chipu wamejawa na imani watafanya vyema katika mashindano ya Barthes Trophy yanayohusisha mataifa manne – Kenya, Namibia, Tunisia na Senegal.

Kenya itavaana na Tunisia nayo Namibia ilimane na Senegal katika mechi za nusu-fainali mnamo Aprili 4. Washindi wataingia fainali itakayosakatwa Aprili 7 saa kumi jioni baada ya mechi ya kuamua nambari tatu itakayokutanisha timu zitakazopoteza katika nusu-fainali. Timu itakayovuta mkia itapoteza nafasi yake katika mashindano haya ya daraja ya juu kabisa (Kundi A).

Odera ametaja wachezaji 25 kutoka kwa kikosi cha wachezaji 30 alichokuwa nacho. Amempa unahodha Bonface Ochieng’ kutoka klabu ya Kenya Harlequin. Samuel Asati atakuwa naibu wa nahodha. Wawili hawa wako katika orodha ya wachezaji sita waliokuwa katika timu ya Chipu iliyopoteza 37-18 dhidi ya Namibia katika fainali ya mwaka 2018 jijini Windhoek. Wachezaji wengine ni Emmanuel Silungi, James Mcgreevy, Jeff Mutuku na Michele Brighetti. Vilevile, Mutuku alishiriki makala ya mwaka 2017 ambapo Chipu ilipepetwa 66-24 na Namibia katika fainali nchini Madagascar.

Chipu ilikuwa mwenyeji wa mashindano ya JWRT mwaka 2009. Hata hivyo, imepata ugumu kurejea katika ulingo huo wa dunia mara nyingi tu ikimaliza ya pili barani Afrika nyuma ya Namibia mwaka 2013, 2014, 2016 na 2017 na 2018. Odera na vijana wake wamekuwa wakifanya maandalizi yao tangu Januari 20, 2019 na wanatumai mwaka huu ni wao.

Hata hivyo, bado Namibia inapigiwa upatu kuendeleza ubabe wake. Gazeti la The Namibian lilinukuu Rais wa Shirikisho la Raga la Namibia Corry Mensah akisema Jumatatu kwamba Namibia ina matumaini makubwa kutwaa tiketi ya kuwakilishi bara Afrika katika mashindano ya JWRT ya mwaka 2019 yatakayofanyika nchini Brazil mnamo Julai 9-21.

Namibia ya kocha Johan Diergaardt itakuwa ikifukuzia tano la tano mfululizo la Afrika. Diergaardt ametaja wachezaji 15 wapya katika kikosi chake kinachotarajiwa jijini Nairobi mnamo Jumanne alasiri. Senegal na Tunisia zilitarajiwa jijini Nairobi mapema Jumanne.

Kikosi cha Chipu:

Ian Njenga (Nondescripts)

Bonface Ochieng’ (Nahodha/Kenya Harlequin)

Rotuk Rahedi (Millfield College)

Emmanuel Silungi (Homeboyz)

Hibrahim Ayoo (Menengai Oilers)

James Mcgreevy (Kenya Harlequin)

Brian Amaitsa (Nondescripts)

Darren Kahi (Blak Blad)

Samuel Asati (Nahodha msaidizi/KCB)

Dominic Coulson (Hana klabu)

Beldad Ogeta (Menengai Oilers)

Owain Ashley (Merchiston Castle)

George Maranga (KCB)

Geoffrey Okwach (KCB)

Jeff Mutuku (Kenya Harlequin)

Wilfred Waswa (Northern Suburbs)

Collins Obure (Blak Blad)

Ian Masheti (Impala Saracens)

Frank Aduda (Impala Saracens)

George Kiryazi (Merchiston Castle)

Samuel Were (Laiser Hill Academy)

Barry Young (Kabras Sugar)

Douglas Kahuri (Kenya Harlequin)

Michele Brighetti (Sedburgh School)

Andrew Matoka (Strathmore University).