Michezo

Kocha Ole Gunnar ajivunia pasi za Bruno

February 5th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

MANCHESTER, Uingereza

KOCHA wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer amemlinganisha kiungo mpya, Bruno Fernandes na staa wa zamani wa klabu hiyo, Paul Scholes kuliko Cristiano Ronaldo.

Bruno, 25, alisajiliwa majuzi akitokea klabu ya Sporting Lisbon ya Ureno.

Alicheza mechi ya kwanza ya Ligi Kuu ya Uingereza( EPL) mwishoni mwa wiki dhidi ya Wolves, wakitoka sare ya 0-0 uwanjani Old Trafford.

Lakini baada ya kumchunguza kwa makini mazoeni na pia uwanjani wakati wa mechi, Solskjaer amesema nyota huyo ana sifa nyingi za kiungo wa zamani Scholes, kuliko mshambuliaji Cristiano Ronaldo wa Juventus, ambaye pia aliwahi kutamba pale Old Trafford.

“Namtakia Bruno maisha mema hapa klabuni, nikimtarajia afaulu pakubwa baada ya kumshuhudia akipiga makombora makali hata wakati wa mazoezi.

“Nimependa juhudi zake za kupika pasi fupi fupi na hata zile ndefu,” alieleza Solskjaer.

“Namfananisha na Scholes kwa sababu anapambana, anachukia kupoteza mipira na anatumia jezi inayofanana na aliyopenda Scholes. Ni mchezaji aliye na uchezaji wa aina yake. Nina hakika atatuongezea ukwasi ambao tumeukosa msimu huu.”

Mbali na Fernandes, Man-United pia ilifanikiwa kumpata straika Odion Ighalo kutoka klabu ya Shanghai Shenhua, China, kwa mkopo.

Hata hivyo, mkataba wa mshambuliaji huyo raia wa Nigeria hauna kipengele kinachoipa Man-United fursa ya kumnunua kwa muda mrefu.

Ighalo, 30, aliwahi kuchezea Watford ya ligi ya EPL kati ya 2014 na 2017, ambako alifunga mabao 16 katika mechi 55 kabla ya kuelekea China.

Alijiunga kwanza na klabu ya Changchun Yatai kabla baadaye kuyoyomea Shanghai Shenhua mnamo Februari 2019.

Anatarajiwa kuziba pengo la Marcus Rashford anayeuguza jeraha.

Kabla ya kufanikiwa kumnasa straika huyo, Man-United pia walikuwa wak jaribu kumsajili Joshua King wa Bournemouth, lakini ofaa yao ikakataliwa.

Akiwa na timu ya taifa ya Nigeria katika michuano ya kuwania nafasi ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon), Ighalo alifunga mabao saba, kabla ya kufunga mengine matano wakati wa fainali zenyewe nchini Misri.

Kabla ya United kufanikiwa kumpata, nyota huyo kadhalika alikuwa akiwindwa na timu za Tottenham Hotspur na Inter Milan ya Serie A nchini Italia.