Michezo

Kocha Pasuwa wa Big Bullets ya Malawi akataa ofa ya kuinoa AFC Leopards

June 1st, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

MKUFUNZI wa kikosi cha Big Bullets cha Ligi Kuu ya Malawi, Callisto Pasuwa amekataa ofa ya kujiunga na mabingwa mara 13 wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL), AFC Leopards.

Leopards wanatafuta kocha mrithi wa Andre Casa Mbungo, mkufunzi mzawa wa Rwanda aliyeagana nao mwaka 2019.

Zaidi ya Leopards, vikosi vingine vinavyofukuzia maarifa ya Pasuwa ni Dynamos ya Zimbabwe inayowania upya huduma zake.

Nyota ya Pasuwa ilianza kung’aa katika ulingo wa ukufunzi tangu aaminiwe fursa ya kudhibiti mikoba ya Dynamos mnamo 2010.

Chini yake, kikosi hicho kilijitwalia mataji manne ya Ligi Kuu ya Zimbabwe (Castle Lager) kati ya 2011 na 2014.

Rekodi hiyo nzuri ilimpa nafasi ya kuinoa timu ya taifa ya Zimbabwe almaarufu ‘The Warriors’ na akakisaidia kikosi hicho kufuzu kwa fainali za Kombe la Afrika (AFCON) 2017 zilizoandaliwa nchinI Gabon.

Mwishoni mwa fainali hizo, Pasuwa alitua kambini mwa Big Bullets ambao kwa sasa amewaongoza kunyanyua mataji mawili ya Ligi Kuu katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.