Michezo

Kocha Patrick Vieira afutwa kazi baada ya matokeo duni ya kikosi cha Nice

December 5th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

KLABU ya Nice inayoshiriki Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) imemfuta kazi kocha Patrick Vieira baada ya kipindi cha miaka miwili na nusu.

Kiini cha kutimuliwa kwa kiungo huyo wa zamani wa Arsenal na timu ya taifa ya Ufaransa ni msururu wa matokeo duni yaliyosajiliwa na Nice.

Nice walipoteza jumla ya michuano mitano iliyopita kwa mfululizo, ukiwemo ule wa Europa League uliowashuhudia wakipokezwa kichapo cha 3-2 kutoka kwa Bayer Leverkusen waliowabandua kwenye kipute hicho.

Kufikia sasa, Nice wanashikilia nafasi ya 11 kwenye msimamo wa jedwali la Ligue 1.

Vieira ambaye aliwahi kuchezea Manchester City, Inter Milan na Juventus, aliwahi pia kudhibiti mikoba ya kikosi cha New York City nchini Amerika kabla ya kuajiriwa na Nice.

Adrian Ursea ambaye alikuwa msaidizi wa Vieira sasa amepokezwa rasmi mikoba ya Nice.