Kocha Rangnick asema mvamizi Martial alikataa kuchezea Man-United dhidi ya Aston Villa

Kocha Rangnick asema mvamizi Martial alikataa kuchezea Man-United dhidi ya Aston Villa

Na MASHIRIKA

KOCHA mshikilizi wa Manchester United, Ralf Rangnick, amesema fowadi Anthony Martial alikataa kuwajibishwa katika mchuano wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ulioshuhudia mabingwa hao mara 20 wa kipute hicho wakiambulia sare ya 2-2 dhidi ya Aston Villa mnamo Jumamosi usiku ugani Villa Park.

Martial, 26, alimweleza Rangnick kuhusu mpango wake wa kuondoka kambini mwa Man-United mwezi huu na nyota huyo raia wa Ufaransa anahusishwa pakubwa na uwezekano wa kuyoyomea Uhispania kuvalia jezi za Sevilla.

Martial hajawahi kuanza mechi yoyote ya EPL tangu Oktoba 2 na hajachezea kikosi hicho katika pambano lolote tangu Disemba 2, 2021 Man-United walipokomoa Arsenal 3-2.

Wingi wa visa vya majeraha, maambukizi ya virusi vya corona na idadi kubwa ya wanasoka wanaowakilisha mataifa yao kwenye fainali za Kombe la Afrika (AFCON) nchini Cameroon ni miongoni mwa sababu zilizomchochea Rangnick kutaka kuchezesha Martial dhidi ya Villa.

“Niliuliza iwapo atakuwa radhi kujaza mojawapo ya mapengo lakini akakataa,” akasema Rangnick.

Martial amefungia Man-United mabao 56 kutokana na mechi 173 za EPL. Makali yake ugani Old Trafford yalishuka pakubwa kuanzia 2018 chini ya aliyekuwa mkufunzi wa Man-United, Jose Mourinho ambaye sasa anadhibiti mikoba ya AS Roma nchini Italia.

Mnamo Januari 2019, Martial alitia saini mkataba mpya wa hadi 2024 kambini mwa Man-United chini ya mkufunzi raia wa Norway, Ole Gunnar Solskjaer.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Naunga Raila kwa sasa ila macho yangu yako kwa urais 2027...

Okutoyi aduwazwa na mnyonge Australia, asema ni funzo

T L