Kocha Thomas Tuchel aanza kazi kambini mwa Chelsea baada ya kuaminiwa kuwa mrithi wa Lampard

Kocha Thomas Tuchel aanza kazi kambini mwa Chelsea baada ya kuaminiwa kuwa mrithi wa Lampard

Na MASHIRIKA

CHELSEA wamemteua kocha wa zamani wa Paris Saint-Germain (PSG), Thomas Tuchel kuwa mkufunzi wao kwa kipindi cha miezi 18 ijayo.

Hata hivyo, mabingwa hao wa zamani wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) watakuwa huru kurefusha mkataba wa Tuchel kutegemea matokeo yake.

Akiwa PSG, Tuchel ambaye ni raia wa Ujerumani, alisaidia miamba hao kutia kapuni makombe mawili ya Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1), taji la French Cup na French League Cup.

“Siwezi kusubiri zaidi kuanza kudhibiti mikoba ya Chelsea katika EPL – ligi iliyo na ushindani mkali zaidi duniani. Nafurahia kuwa sehemu ya kikosi hiki,” akasema Tuchel, 47.

Chelsea walimfuta kazi mkufunzi Frank Lampard mnamo Januari 25 baada ya kuhudumu uwanjani Stamford Bridge kwa miezi 18 akiwa kocha. Kiini cha kutimuliwa kwake ni matokeo duni ya Chelsea waliosajili ushindi mmoja pekee kutokana na miezi mitano mfululizo ya EPL.

“Sote tunamheshimu Lampard na kazi ambayo ameifanya uwanjani Stamford Bridge kufikia sasa. Amebadilisha kikosi na kuleta moyo wa ushindani miongoni mwa wachezaji,” akaongeza Tuchel ambaye pia amewahi kuwatia makali vijana wa Borussia Dortmund.

Tuchel anakuwa mkufunzi wa 11 kuajiriwa na Chelsea tangu bwanyenye mzawa wa Urusi na raia wa Israel, Roman Abramovich atwae umiliki wa kikosi hicho mnamo 2003.

“Tuchel ni miongoni mwa wakufunzi bora zaidi katika soka ya bara Ulaya kwa sasa. Tuna matarajio makubwa kutoka kwake na ninaamini atatuongoza kufikia mengi ya malengo yetu msimu huu na hata baadaye,” akasema mkurugenzi wa michezo kambini mwa Chelsea, Marina Granovskaia.

Kibarua cha kwanza cha Tuchel kambini mwa Chelsea ni mchuano wa EPL utakaowakutanisha waajiri wake na Wolves uwanjani Stamford Bridge mnamo Januari 27, 2021.

Lampard ambaye ni kiungo wa zamani wa Chelsea, ndiye mfungaji bora wa muda wote kambini mwa kikosi hicho. Mchuano wake wa mwisho kusimamia katika kikosi cha Chelsea ni ule ulioshuhudia masogora wake wakisajili ushindi wa 3-1 dhidi ya Luton Town kwenye raundi ya nne ya Kombe la FA uwanjani Stamford Bridge.

Lampard aliteuliwa kuongoza Chelsea kwa mkataba wa miaka mitatu mnamo Julai 2019 baada ya kuaminiwa fursa ya kuwa mrithi wa Maurizio Sarri. Katika msimu wake wa kwanza wa ukocha, Chelsea waliambulia nafasi ya nne kwenye EPL na wakatinga fainali ya Kombe la FA ambapo walizidiwa ujanja na Arsenal waliowachapa 2-1 uwanjani Wembley, Uingereza.

Ushindi wa 3-1 dhidi ya Leeds United mwanzoni mwa Disemba 2020 uliwaweka Chelsea kileleni mwa jedwali la EPL. Hata hivyo, kushindwa kwao katika mechi tano kati ya nane zilizopita kuliwateremsha hadi nafasi ya tisa kwa alama 29 sawa na West Ham United ya kocha David Moyes.

Tuchel anaanza kazi kambini mwa Chelsea miezi mitano baada ya kuongoza PSG kutinga fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kwa mara ya kwanza. Hata hivyo, walipigwa 1-0 na Bayern Munich waliotwaa ufalme wa taji hilo mnamo 2019-20 jijini Lisbon, Ureno.

Tuchel amewahi pia kunoa vijana wa Mainz na Borussia Dortmund alikorithi mikoba iliyokuwa ikishikiliwa na kocha wa sasa wa Liverpool, Jurgen Klopp.

Kati ya wanasoka aliowahi kuwanoa kambini mwa vikosi hivyo ni Christian Pulisic (Chelsea), Ousmane Dembele (Barcelona) na Pierre-Emerick Aubameyang (Arsenal).

Tuchel alifutwa kazi na PSG mnamo Disemba 24, 2020. Wakati huo, miamba hao wa soka ya Ufaransa walikuwa wakishikilia nafasi ya tatu kwenye msimamo wa jedwali la Ligue 1 baada ya kupoteza jumla ya michuano minne ligini.

You can share this post!

Arsenal wapepeta Southampton na kutinga ndani ya orodha ya...

Sofapaka yatema wanasoka wanane