Kocha Tuchel asema atasalia Chelsea hadi mwisho wa msimu huu

Kocha Tuchel asema atasalia Chelsea hadi mwisho wa msimu huu

Na MASHIRIKA

KOCHA Thomas Tuchel amesema ana wajibu wa pamoja na wachezaji wake kupigania maslahi ya kila mfanyakazi kambini mwa Chelsea huku akiapa kwamba atasalia kudhibiti mikoba ya kikosi hicho hadi mwisho wa msimu huu wa 2021-22.

Katika mchuano wao wa kwanza tangu mmiliki wao Roman Abramovich awekewe vikwazo na kupigwa marufuku ya kuwa mkurugenzi wa Chelsea, miamba hao walitandika Newcastle United 1-0 katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ugani Stamford Bridge mnamo Jumapili.

Siku hiyo hiyo, vipusa wa Chelsea wanaonolewa na kocha Emma Hayes walikomoa warembo wa Aston Villa 1-0 katika Ligi Kuu ya Soka ya Wanawake nchini Uingereza (WSL).

Sawa na Petr Cech ambaye ni mshauri mkuu wa benchi ya kiufundi, Tuchel amehakikishia mashabiki wa Chelsea kwamba hataondoka ugani Stamford Bridge hadi mwishoni mwa msimu na kubwa zaidi kwa sasa ni “kuchukulia mambo hatua kwa hatua”.

“Nitasalia hapa hadi mwishoni mwa msimu. Lazima tusubiri matukio ya siku hadi siku kwa sababu huenda mambo yakabadilika na kila kitu kikawa shwari. Tuna maswali mengi kuliko majibu. Lakini lazima tuungane na wachezaji kupigania haki ya kila mmoja kambini,” akasema Tuchel.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Afueni kaunti ikizindua kituo cha upasuaji

Msako mkali dhidi ya disko matanga kuanza

T L