Michezo

Kocha wa Ingwe awazia kujiuzulu baada ya kichapo

July 23rd, 2018 1 min read

Na CECIL ODONGO

KOCHA wa AFC Leopards Rodoflo Zapata huenda alisimamia mechi yake ya mwisho na timu hiyo katika kichapo cha 2-1 mikononi mwa Mabingwa watetezi wa KPL Gor Mahia kwenye debi ya ‘Mashemeji’  Jumapili 22.

Mkufunzi huyo alikataa kubainisha wazi hatima yake katika kambi ya ‘Ingwe’ wakati akishiriki mahojiano baada ya debi hiyo huku akisisitiza kwamba ataandaa mkutano na Mwenyekiti wa AFC Leopards Dan Mule kabla hajazamia matayarisho ya  michuano ijayo.

“Sijui. Nitakutana na mwenyekiti kwanza. Hapo ndipo nitazungumza chochote kuhusu mechi zetu zijazo,” akasema Zapata.

Inasemekana raia huyo wa Argentina huenda akajiuzulu baada ya taarifa kuibuka kwamba haonani uso kwa macho na baadhi ya maafisa wa ‘Ingwe’ anaodai wanatumia benchi yake ya kiufundi kumhujumu kikazi kwa kuwa hawapendezwi na mbinu na sera zake za ukufunzi.

Zapata alichukua usukani wa kuinoa AFC Leopards Mwezi Mei, 2018 na alikuwa kwenye benchi ya kiufundi wakati wa mechi ya Kombe la Super Cup uwanjani Afraha ambapo Gor Mahia walikipiga kikosi chake 1-0.

Kichapo cha Jumapili kilikuja siku chache tu baada ya Zapata kuchokoza Gor Mahia kwa kudai ‘Ingwe’ ndiye klabu bora yenye mashabiki wengi nchini.