Michezo

Kocha wa Kakamega Homeboyz afichua mbinu aliyotumia kuigaragaza Tusker

May 28th, 2018 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA wa Kakamega Homeboyz, Mike Mururi hatimaye amefichua siri aliyotumia kuizima timu ya kocha mwenzake Robert Matano, Tusker 2-0 uwanjani Ruaraka.

Mururi alisema mbinu zake zilizaa matunda dhidi ya Tusker, ambao kwa sasa wamepoteza mechi tatu mfululizo dhidi ya timu ilizozizidi kwa uzoefu wa ligi.

Kiungo wa zamani wa Green Commandos na Western Stima Eston Esiye alitia kimiani boa la ufunguzi kabla ya kummegea straika wa zamani wa Tusker Allan Wanga ambaye alimalizia ka kufanya mambo kuwa 2-0.

Ushindi huo ulimaliza ukame wa Homeboyz wa kushinda dhidi ya Tusker ambapo wamepoteza mara 5 katika mechi 6 walizopatana ligini.

Kocha huyo wa zamani wa Chemelil ana furaha baada ya kuwaagiza vijana wake kumiliki mpira katika ngome ya Tusker.

 

“Nina raha kutokana na ushindi huu – mbinu zetu zilienda kama tulivyopanga. Kabla ya mechi, niliwaambia vijana wangu waishambulie Tusker katika ngome yao, kwa kuwa uwanja huo uko katika hali duni, na ingekuwa vigumu kwetu kujaribukucheza katika ngome yetu. Pia nilijua Tusker ilikuwa na presha na ingekuwa rahisi kuwapiga bao, na hicho ndicho kilitokea,” akasema baada ya mechi.

Kocha huyo alikuwa anasemekana kugura klabu hiyo  huku tetesi zikisema angeelekea Vihiga United lakini Homeboyz wakafanikiwa kumshawishi kusalia humo.Ameiongoza timu yake kushinda mechi saba msimu huu.