Michezo

Kocha wa KCB atamani kuepuka Gor ashinde Sportpesa Shield

April 2nd, 2019 1 min read

NA CECIL ODONGO

NAIBU Mkufunzi wa KCB Sammy ‘Pamzo’ Omollo amesema lengo kubwa la timu hiyo msimu huu ni kutwaa Kombe la Ngao ya Sportpesa ili kuwakilisha taifa kwenye soka ya Bara Afrika msimu wa 2019/2020.

Wanabenki hao walifuzu hatua ya robo fainali ya kipute hicho Jumamosi Machi 30 pale walipoichabanga Vihiga Sportif mabao 4-0 kwenye mchuano wa mwoondoano uliosakatwa katika uwanja wa Kenyatta mjini Machakos.

Hata hivyo, kocha huyo wa zamani wa Tusker na Posta Rangers alisema ndoto yao ya kutwaa ubingwa itatimia tu iwapo wataepuka kukutanishwa na Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu(KPL) Gor Mahia katika hatua za robo fainali au nusu fainali.

“Tuko na nafasi murwa ya kutinga fainali ya kipute cha Sportpesa Shield kwa mara ya kwanza kwenye historia ya klabu msimu huu. Hata hivyo lazima tuombe tusikutanishwe na Gor Mahia katika awamu ya nusu na robo fainali hadi tufike fainali. Iwapo tutakutanisha nao basi huenda mambo yakawa magumu zaidi kwetu,”

“Hata hivyo itakuwa bora tukikutana nao kwenye fainali kwasababu hapo kila timu ina uwezo wa kushinda na kubeba taji. Kikosi kiko sawa na tunalenga sana kutwaa taji hilo msimu huu,” akasema Omollo.

Bingwa mtetezi wa Kombe hilo ni Kariobangi Sharks ambao pia tayari wamefuzu kwa awamu ya robo fainali. Mshindi wa taji hilo hupata nafasi ya kuwakilisha taifa katika mashindano ya Kombe la Mashirikisho Barani Afrika(CAF).