Michezo

Kocha wa Kenya Morans apuuzilia mbali anajiunga na APR Rwanda

November 15th, 2020 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

KOCHA wa timu ya taifa ya mpira wa vikapu ya wanaume ya Kenya Morans, Cliff Owuor amekana ripoti zinazomhusisha na kurejea klabu ya APR.

Owuor aliongoza APR kati ya mwaka 2005 na 2016 akishinda nayo Ligi Kuu ya Rwanda mara nne pamoja na kutwaa taji moja la Afrika Mashariki na Kati (Zone 5).

Akizungumza na Taifa Leo kwa njia ya simu Jumapili, Owuor alionekana kushtushwa na habari katika gazeti moja maarufu nchini Rwanda lililodai kuwa amewasiliana na viongozi wa APR na yuko pua na mdomo kufikia mapatano.

“Sina habari. Huo ni uvumi tu kwa sababu sijawasiliana na APR, Nitawasiliana na klabu hiyo nipate kujua habari hizo zinatoka wapi,” alisema Owuor na kuongeza kuwa umakinifu wake wote uko katika kuongoza Morans kwenye mashindano ya kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (AfroBasket) yatakayofanyika jijini Kigali juma lijalo.

Gazeti la New Times Rwanda liliripoti Novemba 11 kuwa kwa majuma kadhaa sasa Owuor amekuwa akizungumza na APR likiongeza kuwa Mkenya huyo atajiunga na miamba hao wiki chache zijazo kwa sababu “ameshaafikiana matakwa ya kibinafsi na klabu hiyo’.

Owuor alikuwa usukani Morans ikiandikisha historia kwenye mashindano ya Bara Afrika ya wachezaji wanaocheza barani Afrika almaarufu AfroCan kwa kuzoa medali ya fedha jijini Bamako nchini Mali mwaka 2019.

Kwa sasa, anaandaa Morans jijini Nairobi kupigania mojawapo ya tiketi tatu mezani za kuingia AfroBasket2021. Morans itamenyana na wakali wa Senegal (Novemba 25), Angola (Novemba 26) na Msumbiji (Novemba 27) katika mechi za Kundi B jijini Kigali.

Vijana wa Owuor watarudiana na wapinzani hawa tena kati ya Februari 19 na Februari 21 mwaka 2021. Timu tatu za kwanza baada ya michuano hiyo yote kusakatwa zitatinga dimba la AfroBasket litakalofanyika jijini Kigali baadaye 2021. Kenya ilishiriki AfroBasket mara ya mwisho miaka 27 iliyopita.