Michezo

Kocha wa KNH alenga kushinda mechi zilizosalia na kumaliza kileleni

May 28th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

KOCHA wa timu ya Hospitali Kuu ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH), George Makambi anaamini kikosi chake kina fursa ya kufanya vizuri kwenye mechi za Kundi A Ligi ya Taifa Daraja ya Pili msimu huu.

‘Sina budi kutaja kwamba kampeni za mwaka huu ni moto lakini nashukuru tunazidi kujikaza,” alisema na kuongeza kwamba wamepania kushinda mechi zote zilizosalia ili kumaliza kileleni na kunasa tikiti ya kufuzu kushiriki mechi za Ligi ya Taifa Daraja ya Kwanza msimu ujao.

Kocha huyo alisema wameshiriki Daraja ya Pili kwa muda mrefu ambapo itakuwa vizuri kwa kikosi kufuzu kushiriki ligi ya juu.

Wanasoka wa KNH walipanda hatua mbili mbele na kutua nafasi ya nne kwa alama 30 walipotuzwa alama tatu bila jasho baada ya Mwiki United kuingia mitini.

Nayo Uweza FC ambayo hunolewa na kocha, Charles ‘Stam’ Kaindi iliibugiza Commercial FC mabao 2-1 kwenye patashika iliyopigiwa uwanjani Woodley Kibera, Nairobi. Kocha huyo alipongeza vijana wake kwa kujitahidi na kuzima wapinzani wao.

Kwenye mechi nyingine, Balaji EPZ ilipigwa breki ilipolazimisha kutoka sare ya bao 1-1 na Limuru Olympics, Maafande wa Thunder Bird walichomwa mabao 2-1 na Thika Allstars, Kenafric FC ilikandamiza Jumbo T kwa magoli 6-1 nayo Zetech University FC iliandikisha ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Magana Flowers.

Katika msimamo wa kinyang’anyiro hicho, Balaji EPZ ingali kifua mbele kwa kufikisha alama 36, moja mbele ya Uweza FC. Mwiki United imetinga nafasi ya tatu kwa alama 31, moja bele ya KNH huku Zetech University ikizoa alama 29 na kufunga tano bora.