Michezo

Kocha wa Laiser Hill aapa kufunza wapinzani gozi Chapa Dimba

April 17th, 2020 2 min read

Na JOHN KIMWERE

WAVULANA wa kikosi cha Laiser Hill Academy wamepania kutifua vumbi la kufa mtu kwenye fainali za kitaifa kufukuzia ubingwa wa taji la Chapa Dimba na Safaricom Season Three. Kocha wake, Anderson Sango amesema ingawa itakuwa mara ya kwanza kwa chipukizi wake kushiriki fainali za kitaifa ana imani wametosha mboga kujikakamua na kufanya vizuri.

Laiser Hill Academy itashiriki ngarambe hiyo baada ya kuibuka bingwa wa kipute hicho katika Mkoa wa Bonde la Ufa mwaka huu. Wavulana hao wabeba ubabe wa eneo hilo msimu licha ya kushindwa maarifa na wapinzani wao katika fainali za makala ya pili mwaka uliyopita.

”Tunafahamu bayana kuwa fainali za muhula huu zitakuwa balaa maana timu zote zimejiandaa kiume kukabili wapinzani kwa udi na uvumba kusaka ubingwa wa kitaifa,” anasema kocha huyo na kuongeza kuwa wanalenga kushiriki mazoezi makali baada ya shughuli kurejea kawaida.

Alex Karani wa Laiser Hill Academy akipiga mpira kumkwepa Kevin Amdavi wa Tumkas kwenye nusu fainali ya Chapa Dimba na Safaricom Season Three iliyopigiwa Green Stadium, Kericho. Laiser Hill ilishinda mabao 2-0.

Alidokeza hayo kwa kuzingatia shughuli za michezo kote nchini zimesitishwa kufuatia mlipuko wa virusi hatari vya korona. Kadhalika alisema kwenye kinyang’anyiro hicho watashiriki kila mechi kama fainali wala hawawezi kupuuza wapinzani wao.

MABINGWA WA MKOA

Laiser Hill Academy chini ya manahodha, Timothy Ouma na Byran Otieno ilijikatia tiketi ya kusonga mbele ilipobamiza wapinzani wao katika fainali.

Alfred Tanui wa Kapenguria Heroes (kushoto) akishindana na John Williams wa White Rhino kwenye nusu fainali ya Chapa Dimba na Safaricom Season Three iliyopigiwa Green Stadium, Kericho. Kapenguria Heroes ilishinda mabao 2-1.

Kikosi hicho kilibugiza Kapenguria kwa magoli mabao 4-2 kwa mikwaju ya penalti baada ya kuagana sare ya bao 1-1 katika muda wa kawaida. Kwenye nusu fainali, Kapenguria iliilemea White Rhino kwa mabao 2-1 nao chipukizi wa Laiser Hill Academy walitwaa mabao 2-0 dhidi ya Tumkas ya Uasin Gishu waliofunga kupitia Stephene Owino na Timothy Owino. Wavulana hao walizoa tiketi ya kushiriki fainali za Mkoa huo baada ya kushusha ushindani wa kweli na kushinda jumla ya mechi 13.

Timothy Ouma mchezaji wa Laiser Hill Academy alijizolea tuzo ya mchezaji anayeimarika kitengo cha wavulana. Naye mchana nyavu mwepesi Muimi James wa Laiser Hill na Alfred Tanui (Kapenguria Heroes) waliibuka mnyakaji bora na mfungaji bora mtawalia.

Isaac Teigong (kushoto) wa Laiser akishindana na mpinzani wake Alfred Tanui wa Kapenguria Heroes kwenye fainali za Mkoa wa Bonde la Ufa za taji la Chapa Dimba na Safaricom Season Three.

TIKETI

Huku ikiwa zimesalia fainali za maeneo mawili: Mkoa wa Magharibi na Nyanza tayari timu sita zimenasa tiketi ya kushiriki fainali za kitaifa ambazo kabla ya mkurupuko wa virusi vya korona zilikuwa zimepanga kuandaliwa mwezi Juni mjini Mombasa.

Orodha ya vikosi hivyo inajumuisha: Laiser Hill Academy (Mkoa wa Bonde la Ufa), Berlin FC (Mkoa Kaskazini Mashariki), Ulinzi Youth (Mkoa wa Kati), Dagoretti Mixed (Mkoa wa Nairobi), Tumaini School (Mkoa wa Mashariki) na Yanga FC kutoka Malindi Mkoa wa Mombasa.

Alfred Tanui wa Kapenguria Heroes aliyeibuka mfungaji bora.