Kocha wa Senegal amtaka Klopp aheshimu AFCON

Kocha wa Senegal amtaka Klopp aheshimu AFCON

Na MASHIRIKA

MKUFUNZI wa timu ya taifa ya Senegal, Aliou Cisse, amemcharukia kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp, kwa kudunisha hadhi ya mashindano ya Kombe la Afrika (AFCON).

Kwa mujibu wa Cisse, Klopp anastahili kushukuru wanasoka wa Afrika kwa ukubwa na upekee wa mchango wao katika ufanisi wa Liverpool.

“Klopp yupo alipo kitaaluma kwa sababu ya masogora wa Afrika. Alikuwa akipoteza kila fainali ya haiba kubwa bila wachezaji hao,” akatanguliza Cisse.

“Ilikuwa hadi Liverpool waliposajili Mohamed Salah (Misri), Sadio Mane (Senegal), Joel Matip (Cameroon) na Naby Keita (Guinea) ambapo Klopp alifaulu kunyanyua ufalme wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) na Ligi Kuu ya Uingereza (EPL),” akasema.

“Naongoza timu ya taifa ya Senegal ambayo ina mchezaji anayesakatia Liverpool. Naheshimu Liverpool, si Klopp ambaye anadunisha hadhi ya soka ya Afrika kwa kuita AFCON pambano dogo,” akaongeza.

Kauli ya Cisse inachochewa na matamshi ya Klopp aliyezua hofu kuhusu usalama wa wachezaji wa EPL ambao sasa hawatakuwa na pumziko lolote fupi hadi Machi 2022 baada ya kukamilika kwa fainali za AFCON zitakazoandaliwa Cameroon kati ya Januari na Februari mwakani.

Cisse anashikilia kwamba kipute cha AFCON kinastahili kuchukuliwa kwa hadhi sawa na kivumbi cha bara Ulaya (Euro) ambacho pia hujumuisha mataifa 24.

“Yashangaza kuwa Klopp anadharau kipute cha AFCON ambacho kina kiwango sawa cha washiriki na mapambano ya Euro. Aidha, AFCON itajivunia uwepo wa masupastaa wale wale wanaofanya nyota yake (Klopp) kung’aa pale Liverpool.”

Senegal iliambulia nafasi ya pili nyuma ya Algeria kwenye makala yaliyopita ya fainali za AFCON nchini Misiri mnamo 2019.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

DOUGLAS MUTUA: Bara Afrika linaonewa kwa kugundua kirusi...

Kabras, Strathmore na Menengai Oilers wang’aria wenyeji...

T L