Michezo

Kocha wa Vihiga awatia nari vijana wake kudhidhirisha makali yao ligini

March 14th, 2018 1 min read

Na CECIL ODONGO

NAIBU Kocha wa Klabu ya Vihiga United Francis Xavier amewataka vijana wake kunyanyuka na kupigana kiume ili kupata ushindi wao wa kwanza kwenye ligi kuu ya KPL.

Kocha huyo msaidizi amesikitia matokeo duni ya klabu hiyo hadi sasa na kuhoji kwamba wasipojizatiti kubadili mkondo wa mambo huenda wakaangukiwa na shoka la kutemwa nje ya ligi.

Hata hivyo amesisitiza kwamba maonevu na maamuzi yasiyoridhisha kwenye mechi waliyogaragaza dhidi ya Klabu ya Nakumatt FC yaliwaponza ushindi wao wa kwanza ligini.

“Hapajaharibika jambo bado mechi ni nyingi na nina wingu la matumaini kwamba ushindi wetu wa kwanza ligini unajongeajongea.Mechi dhidi ya Nakumatt ilikuwa wazi tungeshinda lakini hii ni soka na yaliyotokea yalitokea,” akasema.

Hadi sasa timu hiyo kutoka Magharibi mwa nchi imeandikisha sare nne na kupoteza mechi moja  wakiwa wananing’inia kwenye eneo hatari la kuteremshwa ngazi katika nafasi ya 16 kwenye msimamo wa jedwali la ligi.

Walisajili sare tasa dhidi ya klabu za Zoo Kericho, Nakumatt na Posta Rangers huku wakifungwa 2-1 na Kakamega Homeboyz na sare ya 2-2 dhidi ya Kariobangi Sharks.

Wikendi hii klabu hiyo inakaribisha wanapwani Bandari FC mchuano utakaogaragazwa katika uwanja wa Mumias Complex Kaunti ya Kakamega.

Kabla ya kufuzu kujiunga na ligi kuu ya KPL,Vihiga walitawala ligi ya supa na kumaliza katika nafasi ya kwanza mbele ya Wazito FC na Ushuru FC.

Baadhi ya  wachezaji wanaotarajiwa kujizatiti na kuzolea Vihiga alama tatu muhimu ni Mshambulizi Andrew Murunga na wachezaji wa kiungo cha kati Godfrey Oputi na Victor Ayugi.