Michezo

Kocha wa zamani Uganda Cranes, Micho Milutin, afurahi Algeria kunyukwa na kubanduliwa

January 24th, 2024 1 min read

NA LABAAN SHABAAN

ALIYEKUWA Kocha wa Uganda Cranes, Milutin ‘Micho’ Sredojevic, 54, ametia chumvi kwenye kidonda cha Algeria baada ya timu hiyo kuaibishwa na kichapo kichungu na Mauritania Jumanne usiku.

Algeria ilitimuliwa nje ya Dimba la Kandanda la Afrika (AFCON) 2023 linaloendela nchini Ivory Coast.

Micho angali na kisasi na Mbweha wa Jangwani (Desert Foxes) akikumbuka ni wao waliikosesha timu ya taifa ya Uganda – Uganda Cranes – tiketi ya kushiriki Kombe la Afrika 2023 walipokabana koo katika awamu ya kufuzu.

“Sasa mmehisi vile Waganda milioni 50 walihisi mlipotuchapa,” alisema Micho kupitia sehemu ya chapisho katika akaunti yake ya mtandao wa X (awali Twitter).

Kisha akatania: “Mlichopika Septemba Mwenyezi Mungu amewaandalia Januari. Kandanda ni mchezo ‘mkatili’ na sasa angalau mnahisi Uganda walivyohisi Septemba mkidhani mtaepuka.”

Micho anakisia Algeria ‘walikula njama’ na Tanzania ili watoke sare na wote wafuzu kushiriki AFCON kwa hasara ya Uganda katika mechi ya mwaka wa 2023.

Wakati huo, Uganda waliwapara Niger 2 – 0 katika mechi ya kufuzu na wangeshiriki makala haya kama Algeria ingelima Tanzania mnamo Septemba 7, 2023 katika Kundi F.

Micho sasa ni Kocha wa timu ya taifa ya Libya.

Aliwahi kufunza Chipolopolo ya Zambia na klabu za kandanda Afrika Kusini, Tanzania na Saudi Arabia.