Habari

Kodi: Serikali yalenga 'mahasla'

January 3rd, 2020 2 min read

Na BENSON MATHEKA

HALI ya maisha inatarajiwa kuwa ngumu hata zaidi kwa Wakenya wanaotegemea biashara za mitaani baada ya serikali kuanza kuwatoza ushuru kwa mauzo wanayopata ili kupata pesa za kulipa madeni.

Tayari, serikali imeanza kuwatoza ushuru wa moja kwa moja wamiliki wa biashara ndogo ndogo kama vinyozi, mama mboga na sekta ya Juakali licha ya hali ngumu ya kiuchumi ambayo Wakenya walipitia mwaka 2019.

Kutozwa ushuru huo wa asilimia tatu kwa mauzo ya kila mwaka kunajiri serikali inapoanza kulipa deni la kujenga reli ya kisasa kutoka Mombasa hadi Nairobi.

Bei za bidhaa na huduma katika sekta ya jua kali zitapanda kufuatia ushuru huo mpya ulioanza kutekelezwa jana.

Ushuru huo unatokana na sheria ya fedha ya 2019 ambayo Rais Uhuru Kenyatta aliidhinisha Novemba mwaka jana na unalenga wamiliki ambao mauzo yao ni chini ya Sh5 milioni kwa mwaka.

Ikizingatiwa kuwa mazingira ya kufanya biashara Kenya yamekuwa yakidorora kutokana na sera za serikali, kuwakamua wafanyabiashara wadogo kwa kuwatoza ushuru kutawaumiza zaidi.

Kulingana na Maurice Oray, Naibu Kamishna anayesimamia sera ya biashara katika KRA, lengo la serikali ni kuongeza idadi ya walipa ushuru.

“Jambo muhimu ni kusajili walipa ushuru wengi iwezekanavyo katika kiwango hiki ambao wamekuwa wanakwepa kulipa kodi,” Oray aliambia gazeti la ‘Business Daily’.

Ushuru huo umeanza kutozwa Kenya inapoanza kulipa deni la Sh324 bilioni kujenga reli ya kisasa kutoka Mombasa hadi Nairobi.

Muda wa kulipa deni lilikopwa miaka mitano iliyopita umetimia na awamu ya kwanza inatarajiwa wiki hii kulingana na mkataba wa mkopo kati ya serikali na Exim Bank ya China.

Katika bajeti ya mwaka huu, serikali inatarajia kukopa zaidi ya Sh637 bilioni kujaza pengo katika bajeti ya Sh3.2 trilioni.

Mwaka 2019 dalili zilionyesha kuwa huenda Mamlaka ya Kukusanya Ushuru (KRA) ikakosa kukusanya Sh2.8 trilioni ilivyokadiria, jambo ambalo limefanya Wizara ya Fedha kuongeza kiwango cha deni la humu nchini mwaka huu kutoka Sh301. 7 bilioni hadi Sh514 bilioni.

Hii itafanya mashirika ya kifedha ya humu nchini kunyima wafanyabiashara wadogo mikopo ili yaweze kukopesha serikali hatua ambayo itaendelea kuduwaza ukuaji wa uchumi.

Waziri wa Fedha, Ukur Yatani alithibitisha kuwa serikali itaanza kulipa China pesa ilizokopa kujenga SGR wiki hii. Serikali inatarajiwa kulipa Sh71.4 bilioni kwa mwaka, pesa ambazo itatoa kutoka kwa walipa ushuru kupitia kodi na kufanya maisha kuwa magumu zaidi.

“Tumeanza kulipa na pesa zitakuwa katika akaunti yao wiki ya kwanza ya Januari. Pesa hizo zimetengwa katika bajeti,” Bw Yatani aliambia gazeti la ‘Business Daily’.

Itakuwa hasara kwa Wakenya kwa sababu mapato kutoka huduma katika reli hiyo hayatoshi kulipa mkopo huo. Mapato ya reli hiyo kwa mwezi kwa sasa ni Sh840 milioni ilhali gharama ya kuendesha reli yenyewe ni Sh1.5 bilioni kwa mwezi.

Hata hivyo, Bw Yatani ana matumaini kuwa reli hiyo itaanza kupata faida mwaka 2021.

Rekodi za Wizara ya Fedha zinaonyesha kuwa Kenya itakuwa ikilipa China Sh84.3 bilioni katika mwaka wa 2020/2021 na Sh111.4 bilioni mwaka wa 2021-22 kulipia deni la kujenga reli hiyo pekee.

Kufikia mwishoni mwa mwaka 2019 Kenya ilikuwa na deni la Sh6 trilioni kutoka mashirika mbali mbali ya kifedha ulimwenguni na ya humu nchini na hivyo inatazamiwa kutoza Wakenya ushuru zaidi siku zijazo.