Kimataifa

Kofi Annan kuzikwa nchini Ghana Septemba 13

August 27th, 2018 1 min read

PETER MBURU na MASHIRIKA

ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Kofi Annan ambaye aliaga dunia wiki iliyopita atazikwa na serikali ya taifa lake Ghana, katika Jiji la Accra Septemba 13.

Hii ni kulingana na habari alizotoa Ijumaa rais wa Ghana Nana Akufo-Addo baada ya kukutana na familia ya hayati Annan, akitaja hafla ya mazishi ya kiongozi huyo kuwa ya umuhimu kwa taifa hilo na dunia.

Bw Annan aliaga dunia Agosti 18 akiwa na miaka 80 baada ya kuugua kwa muda mfupi, akiwa nchini Uswizi.

“Alikuwa mmoja wa viongozi wenye umaarufu zaidi katika kizazi hiki, alikuwa kama ndugu yetu mkubwa. Itakua hafla kubwa kwa taifa letu na tunatarajia viongozi wengi kuhudhuria,” akasema Rais Akufo-Addo.

Ni wazi sasa kuwa Bw Annan atazikwa Jijini Accra kwenye kaburi la kijeshi, lililojengwa majuzi.

Kiongozi huyo alizaliwa eneo la Kumasi na kukulia huko kabla ya kufanya kazi na UN kwa takriban miongo minne, akifikia kileleni kama katibu mkuu wa muungano huo.