Michezo

K'Ogalo, Bandari kunyanyuana na wazito wa Afrika

August 27th, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

WAWAKILISHI wa Kenya katika soka ya Afrika, Gor Mahia (Klabu Bingwa) na Bandari (Kombe la Mashirikisho) watalazimika kufanya kazi ya ziada kusalia katika mashindano haya baada ya kukutanishwa na Waarabu katika raundi ya kwanza.

Gor Mahia italimana na USM Alger kutoka Algeria nayo Bandari ivaane na US Ben Guerdane kutoka Tunisia kati ya Septemba 13 na Septemba 29.

Timu ya Gor iliingia hatua hiyo kwa kucharaza Aigle Noir ya Burundi 5-1 uwanjani Kasarani mnamo Jumapili jioni.

Vijana wa Steven Pollack walikuwa wamekabwa 0-0 katika mechi ya mkondo wa kwanza nchini Burundi.

USM Alger ilijikatia tiketi ya kufufua uhasama dhidi ya mabingwa hao wa Kenya kwa kulemea AS SONIDEP kwa kuchapa timu hiyo kutoka Niger 2-1 ugenini na 3-1 Jumapili usiku.

Gor na USM Alger zinafahamiana baada ya kukabiliana katika mechi za makundi za Kombe la Mashirikisho mwaka 2018.

Timu ya Gor ilikabwa 0-0 jijini Nairobi katika mechi ya mkondo wa kwanza kabla ya kulemewa 2-1 nchini Algeria na kubanduliwa nje.

Inamaanisha kuwa Gor itakuwa ikitafuta kulipiza kisasi.

Kitakuwa kibarua kigumu dhidi ya mabingwa hao wa Algeria, hasa kwa sababu Gor ina rekodi mbaya ugenini. Italazimika kufanya kazi kubwa zaidi nyumbani Septemba 13 kabla ya kuzuru Algeria kwa mechi ya marudiano.

Gor itatumia kufikia wakati huo mshambuliaji matata Nicholas Kipkirui atakuwa bado fiti na pia washambuliaji wapya Francis Afriyie (Ghana) na Gislein Yikpe Gnamian (Ivory Coast) watakuwa wameidhinishwa na Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) kushiriki mashindano haya. Walikuwa mashabiki tu dhidi ya Aigle Noir.

Kabla ya kukutana na USM Alger, Gor itakuwa imesakata mechi kadhaa za Ligi Kuu ikiwemo ya kufungua msimu dhidi ya Tusker hapo Septemba 1.

Bandari yapiga hatua moja mbele

Kwa upande wake, mabingwa wa Kombe la Rais wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) Bandari wamepiga hatua moja mbele kutoka kuondolewa katika awamu ya kuingia raundi ya kwanza mwaka 2016 hadi raundi ya kwanza.

Vijana wa Bernard Mwalala wana fursa ya kuenda mbali iwezekanavyo watakapokutana na US Ben Guerdane kwa mara yao ya kwanza kabisa.

Hata hivyo, kusalia kwao mashindanoni kutategemea ikiwa watakuwa wamevumbua mbinu ya kushinda mechi. Sare ya 1-1 dhidi ya Al-Ahly Shendi ya Sudan iliyowezesha Wakenya hao kusonga mbele ilikuwa yao ya tisa katika mechi zake 10 zilizopita katika mashindano yote.

Vijana wa Mwalala watafungua kampeni yao ya ligi dhidi ya Mathare United mnamo Agosti 31.