Michezo

K'Ogalo, Ingwe kusakata mechi zao za ligi KPL

November 30th, 2019 1 min read

Na JOHN ASHIHUNDU

LICHA ya matatizo ya kifedha yanayokumba timu za Gor Mahia na AFC Leopards baada ya wadhamini wao SportPesa kujiondoa, timu hizo zenye ushawishi mkubwa nchini zitafika uwanjani leo Jumamosi kucheza mechi zao za Ligi Kuu nchini (KPL).

Kwenye mechi hizo zitakazoanza saa tisa alasiri, Gor Mahia watakuwa wenyeji wa Ulinzi Stars katika mechi itakayochezewa uwanja wa MISC, Kasarani, wakati AFC Leopards wakisafiri hadi Bunguma kuvaana na Nzoia Sugar ugani Masinde Muliro.

Tayari ukosefu wa kifedha umesababisha kuondolewa ligini kwa klabu ya Nzoia Sugar ambayo ilishindwa kufika uwanjani mara tatu, kinyume na sheria za FIFA.

Ligi kuu ya KPL imekumbwa na wakati mgumu tangu kujiondoa kwa SportPesa, huku timu zikitegemea mashabiki wao.

Imeripotiwa kwamba Gor Mahia na AFC Leopards ambazo zinaendelea kufanya vizuri kwenye ligi hiyo hazijalipa wachezaji wao mshahara wa miezi miwili kufikia sasa.

K’Ogalo wanaongoza msimamo wa ligi hiyo kwa pointi 24, nane mbele ya Ingwe ambao wanashikilia nafasi ya tisa.

Kutokana na hali hii, wachezaji kadhaa wa timu hizo tayari wameaitisha barua za kuwaruhusuwaondoke.

Mlinzi wa Gor Mahia, Maurice Ojwang ni miongoni mwa wachezaji tegemeo wa Gor Mahia anayetaka kuondoka, huku Whyvonne Isuza, Tresor Ndikumana na Vincent Abamahoro wakitaka waachiliwe na Ingwe.

Nahodha akosa kufika mazoezini

Nahodha wa Leopards Soter Kayumba hajafika mazoezini tangu pambano la Mashemeji Derby lichezwe Novemba 10, 2019, ugani MISC, Kasarani.

Akizungmzia hali hiyo, mwenyekiti wa AFC Leopards Dan Shikanda alisema gharama ya klabu hiyo kwa mwezi ni Sh4.2 milioni, huku akiongeza kuwa wanahitaji Sh20 milioni kulipa madeni.

Kwa upande mwingine, mwenyekiti wa Gor Mahia Ambrose rachiel alisema kamati yake inafanya kila juhudi kuhakikisha timu hiyo imepata mdhamini haraka iwezekanavyo.