Michezo

K'Ogalo, Ingwe tayari kupepeta gozi KPL Jumapili

November 9th, 2019 2 min read

Na JEFF KINYANJUI na JOHN ASHIHUNDU

MAKOCHA wote, Andre Casa Mbungo wa AFC Leopards na mwenzake Steven Polack wa Gor Mahia wameeleza kujiandaa vyema kwa pambano la Jumapili, timu hizo zitakapokutana alasiri ugani MISC, Kasarani katika mechi ya Ligi Kuu ya Taifa (KPL).

Ni mechi ambayo imekuja siku chache tu baada ya rekodi ya Gor Mahia ya kutoshindwa kuvunjiliwa mbali na vijana wa Mathare United kwa 1-0 Jumatano kwenye mechi iliyochezewa Kenyatta Stadium, Machakos.

Gor Mahia ambao ndio mabingwa watetezi hadi sasa, wanashikilia nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi hiyo wakiwa na pointi 15 nyuma ya Tusker FC baada ya kujibwaga uwanjani mara sita, huku AFC Leopards wakiwa katika nafasi ya tatu pia kwa pointi 15, lakini baada ya kucheza mechi nane.

Timu hizi zimekutana mara 88, huku Ingwe wakijivunia ushindi mara 26, lakini K’Ogalo wamefanikiwa kushinda 23, mbali na sare mara 39. Mara ya kwanza timu hizo zilikutana ilikuwa mwaka 1968, mechi ambayo Gor Mahia walishindwa kwa 2-1.

Leopards imekuwa na safu nzuri tangu msimu huu uanze baada ya kusajili kipa Benjamin Ochan raia wa Uganda ambaye anashirikiana vyema na mabeki Soter Kayumba, Clyde Senaji, Isaac Kipyegon na Dennis Sikhayi.

Msimu uliopita, katika mikondo miwili, timu hizo zilipokutana, Gor Mahia ilishinda 2-0 na baadaye 3-1 katika mikondo yote.

Mara kwa mara timu hizi zinapokutana, pambano huwa linazua hisia nyingi sana nchini Kenya, sawa na Yanga na Simba SC za Tanzania au Kaizer Chiefs na Orlando Pirates nchini Afrika Kusini.

Uhusiano wa kijamii

Mechi kati ya mahasidi hawa imepewa jina la Mashemeji Derby kutokana na uhusiano wa kijamii wa wafuasi wa timu hizo zenye ushawishi mkubwa nchini Kenya.

Mara kwa mara, Mbungo amekuwa akiwakumbusha mashabiki kwamba lengo lake kubwa ni kiongoza Leopards kutwaa ubingwa wa ligi kuu (KPL) ambao waliutwaa kwa mara ya mwisho mwaka 1998, timu hiyo ilipokuwa chini ya kocha Mtanzania, Sunday Kayuni.

Kwa upande mwingine, kocha Polack amesema vijana wake wamesahau kichapo cha majuzi dhidi ya Matahre na sasa wanalenga kuibwaga Ingwe katika pambano la kesho.

“Tumepanga kuenda huko na kuwaonyesha uwezo wetu uwanjani,” alisema Mwingereza huyo mwenye umri wa miaka 58.