K’Ogalo juu ya meza Tusker wakionja ushindi wa kwanza

K’Ogalo juu ya meza Tusker wakionja ushindi wa kwanza

Na CECIL ODONGO

VIGOGO wa soka nchini Gor Mahia jana walipaa hadi kileleni mwa msimamo wa jedwali la Ligi Kuu huku mabingwa watetezi Tusker wakipata ushindi wao wa kwanza kwa kuiadhibu Wazito 2-1 ugani Ruaraka.Gor ililemea Sofakapaka 1-0 katika mechi iliyoanza mapema ugani MISC Kasarani na sasa imeshinda mechi zote nne za msimu ikiwa na alama 12.Ugani Utalii, KCB ilipata ushindi wake wa pili mfululizo kwa kuipiga Kenya Police 2-1 huku Bidco United ikitoka nyuma na kulazimisha sare ya 1-1 dhidi ya Nzoia Sugar ugani Thika.Katika mtanange mwingine, Nairobi City Stars iliyokuwa ikiongoza ligi wiki nzima iliambulia sare ya 1-1 dhidi ya Posta Rangers ugani Thika.Katika mechi ya Gor, mshambuliaji Jules Ulimwengu, alipachika bao la pekee mnamo dakika ya 24 kwa shuti kali iliyomlemea mnyakaji wa Sofapaka Kevin Omondi kunyaka.Kwa upande mwingine, Shami Kibwana na Deogratious Ojok walifunga bao kila moja na kuipa Tusker ushindi huo wa kwanza baada ya kulemewa 1-0 na 2-1 kwenye mechi zake mbili za mwanzo dhidi ya AFC Leopards na FC Talanta mtawalia.Licha ya Johnmark Makwatta kupachika penalti dakika ya 75 na kusawazisha bao la awali lililofungwa kupitia mpira wa ikabu ya James Mazembe, Kenya Police ilijipata taabani dakika mbili baadaye Henry Onyango kufunga bao la ushindi.Nzoia ilishindwa kulinda uongozi wake wa dakika ya 16 kupitia Kevin Wafula pale ilipomruhusu Jacob Onyango kusawazishia Bidco United kunako dakika ya 83.Brian Marita alifunga bao kutoka yadi 23 kuipa Posta Rangers uongozi kunako dakika ya 36 ila nahodha Anthony ‘Muki’ Kimani akasawazisha dakika ya 52 baada ya kupokezwa pasi na Ezekiel Odera.

You can share this post!

Shujaa yasuasua Safari Sevens ikipamba moto

Walilia vijana kupiga Raila jeki kwa kujisajili kura

T L