Michezo

K'Ogalo yapangua kipute cha kirafiki kati yao na Al Hilal

July 31st, 2019 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

MCHUANO wa kirafiki uliokuwa uwakutanishe mabingwa mara 18 na washikilizi wa taji la Ligi Kuu ya Kenya (KPL), Gor Mahia na Al Hilal ya Sudan jijini Nairobi mnamo Alhamisi ya wiki hii hautapigwa tena.

Haya ni kwa mujibu wa Afisa Mkuu Mtendaji wa Gor Mahia Lordvick Aduda ambaye amethibitisha kuwa miamba hao wa soka ya Sudan wamesitisha mpango wa kufanikisha maandilizi ya mechi hiyo.

Mchuano huo ulikuwa uwe sehemu ya kujifua kwa vikosi hivyo viwili vinavyojizatiti kwa kampeni za kuwania ufalme wa Klabu Bingwa Afrika (CAF Champions League) msimu huu.

Huku Gor Mahia wakijitayarisha kuchuana na Aigle Noir CS ya Burundi, Al Hilal kwa upande wao watapepetana na Rayon Sports ya Rwanda katika raundi ya kwanza ya mchujo wa mikondo miwili.

Kulingana na Aduda, itawalazimu Gor Mahia kwa sasa kutafuta kikosi kingine cha kigeni ili kupimana nguvu nacho kabla ya kushuka dimbani kumenyana na Aigle katika mkondo wa kwanza mnamo Agosti 11.

Mchuano huo utatandazwa ugani Prince Louis, Bujumbura kabla ya marudiano kuandaliwa uwanjani MISC Kasarani, Nairobi wiki moja baadaye.

“Al Hilal walitarajiwa kuwasili humu nchini Jumatatu, lakini hilo lisingewezekana kwa kuwa waliamua Kupiga kambi nchini Misri wanakojiandalia kwa mechi dhidi ya Rayon,” akatanguliza Aduda.

“Kwa sasa tutaandaa kikao na benchi ya kiufundi ili kufanikisha mchuano wa kirafiki na mojawapo ya klabu za haiba kubwa kutoka ugenini,” akaongeza.

Gor Mahia waliondolewa mapema kwenye CAF Champions League msimu jana na hivyo kushuka kuwania ubingwa wa Kombe la Mashirikisho (CAF Confederations Cup) ambapo walibanduliwa na Zamalek SC ya Misri kwenye hatua ya robo-fainali.

 

Wachezaji wa Gor Mahia wajumuika kwa picha ya pamoja kabla ya kuchuana na AS Port ya Djibouti katika mchuano wa kuwania ubingwa wa Cecafa katika uwanja wa Umugunda mjini Rubavu, Rwanda. Picha/ Maktaba

Wanapojizatiti Kupiga hatua kubwa zaidi msimu ujao, watalazimika kuyakosa maarifa ya baadhi ya wachezaji nyota waliowatambisha muhula uliopita. Hao ni Harun Shakava, Francis Kahata na Jacques Tuyisenge ambao kwa sasa wameyoyomea Zambia, Tanzania na Angola mtawalia.

Bandari FC watakuwa wenyeji wa Al Ahly ya Sudan katika mchuano wa mkondo wa kwanza wa Confederations Cup mnamo Agosti 10 jijini Nairobi.

Gor wanatazamiwa kumtuma fowadi wao Francis Mustafa hadi kambini mwa Vipers SC nchini Uganda kwa mkopo wa mwaka mmoja. Hatua hiyo inachochewa na ujio wa wavamizi wawili wa kigeni – Gislein Gnamian wa Ivory Coast na Mghana Francis Afriyie.

Mbali na Mustafa, Gor watalazimika pia kuagana na mchezaji mwingine zaidi wa kigeni, Mganda Hashim Sempala ili kuwapa nafasi sajili wao wapya ambao kimsingi, wanatazamiwa kujaza kikamilifu mapengo ya Kahata na Tuyisenge.

Sempala alijiunga na Gor Mahia mnamo Juni 2018 baada ya kuagana na Tusker ambao kwa sasa wanaziwania upya huduma zake.

Kwenye kampeni za kuwania ubingwa wa taji la CAF katika msimu wa 2017, Gor Mahia walibanduliwa katika raundi ya kwanza na Esperance ya Tunisia, tukio ambalo liliwashuhudia wakishuka ngazi kuwania Kombe la Mashirikisho barani Afrika ambapo walipangwa katika zizi moja na Yanga (Tanzania), USM Alger (Algeria) na Rayon Sports kutoka Rwanda.

Hata hivyo, walishindwa kusonga mbele baada ya kilele cha kundi lao la D kutawaliwa na USM Alger na Rayon waliowazidi maarifa katika mchuano wa marudiano jijini Nairobi.