Michezo

K’Ogalo yapigwa Algeria mashabiki wakimlia refa

March 5th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

KLABU ya Gor Mahia ilipata pigo kubwa katika kampeni ya kuingia robo-fainali ya Kombe la Mashirikisho la Afrika baada ya kupoteza mechi ya pili mfululizo ugenini kwa kuchapwa 1-0 dhidi ya Hussein Dey katika Kundi D nchini Algeria, Jumapili.

Vijana wa Hassan Oktay, ambao walirukia juu ya jedwali walipocharaza Waalgeria hawa 2-0 Februari 24 jijini Nairobi, sasa wameteremka hadi nafasi ya pili.

Walizamishwa na bao kutoka kwa Abderrahmane Yousfi lililopatikana dakika ya tisa uwanjani 5 Juillet 1962 jijini Algiers.

Mabingwa mara 17 wa Kenya, Gor wamesalia na alama sita, moja nyuma ya Hussein Dey, ambayo imerejea kileleni nayo Zamalek, ambayo itaalika Gor jijini Cairo nchini Misri mnamo Machi 10, imezoa alama tano baada ya kupepeta Petro de Luanda nchini Angola 1-0 Jumapili.

Petro iliyolima Gor 2-1 jijini Luanda mnamo Februari 13, inavuta mkia kwa alama nne.

Mechi ya marudiano kati ya Gor na Hussein Dey imewacha mashabiki wa Gor na machungu wakilaani refa Boubou Traore kutoka nchi jirani ya Mali kwa kichapo hicho.

“Refa alitunyima bao la wazi,” alisema shabiki Nelson Omollo Kanyunja.

Gor iliona lango kupitia kichwa cha Mganda Shafik Batambuze kutokana na kona ya Francis Kahata, lakini refa alilikataa kwa sababu lilipatikana kipa Merbah Gaya akiwa amechezewa visivyo.

Kampeni ya Gor kusonga mbele katika mashindano haya ya daraja ya pili ya Afrika sasa inaning’inia baada ya kichapo dhidi ya Hussein Dey.

Gor ilipoteza mara tatu mfululizo dhidi ya Zamalek nchini Misri ikiwemo 4-0 zilipokutana mara ya mwisho nchini humo mwaka 1998 katika raundi ya kwanza ya kipute hiki kwa hivyo itaanza mechi hiyo na asilimia ndogo ya kuishinda.

Vijana wa Oktay, ambao walichapa Zamalek 4-2 jijini Nairobi mapema Februari, watakamilisha mechi za makundi kwa kualika Petro mnamo Machi 17.

Timu mbili za kwanza zitaingia robo-fainali nazo mbili za mwisho zitabanduliwa nje.