Koinange alikuwa kiongozi wa kuaminika, UhuRuto wamwomboleza mbunge

Koinange alikuwa kiongozi wa kuaminika, UhuRuto wamwomboleza mbunge

NA MWANGI MUIRURI

MKUKI katili wa mauti umerejea tena katika bunge la kitaifa na kumvuna mbunge wa Kiambaa Bw Paul Koinange baada ya kuugua ugonjwa wa Covid-19—ugonjwa ambao umeonekana kuwa na makali ya kipekee dhidi ya wanasiasa ambao wamegongwa kwa kiwango kikuu na mauti pamoja na maambukizi.

Bw Koinange aliaga dunia Jumatano asubuhi katika hospitali ya Nairobi na ambapo Rais Uhuru Kenyatta alimwomboleza kama kiongozi wa kuaminika na aliyekuwa na maono thabiti kuhusu wema wa nchi hii.

Alimmtaja mwendazake kama aliyetegemewa katika harakati za kuunganisha taifa na ambapo bungeni, alikuwa mwenyekiti wa kamati kuhusu Utawala na Usalama wa Kitaifa.

Amekuwa mbunge wa Kiambaa tangu 2013 na ambaye alifahamika kwa usiri wa kimaisha kwa njia ya hali ya juu, uzalendo usiotingisika kuhusu taifa na uaminifu mkuu kwa rais na serikali yake.

Kwa msingi huo, Bw Koinange alikuwa ameapa hadharani kuwa “hakuna vile hata iwe namna gani mimi ninaweza nikamuunga mkono Naibu wa Rais Dkt William Ruto na hata siasa zigeuke kwa kiwango gani, wa Dkt Ruto ni mrengo ambao siwezi nikajiunga nao kamwe.”

Alisema kuwa Dkt Ruto alikuwa amemuaibisha katika eneo bunge lake akiwa katika mkutano wa hadhara “alipojifanya hata hanijui kwa jina na akauliza watu wangu huwa wananiita nini wala si nani, hii ikiwa ni baada ya hatua yangu ya kumwambia alikuwa anagawa Wakenya na kampeni zake za mapema na za kukaidi rais Uhuru Kenyatta katika mwito wake kwamba kwanza tuwahudumie Wakenya.”

Hata hivyo, Dkt Ruto amemwomboleza mwendazake kama “kiongozi shujaa na ambaye atakumbukwa na wengi kupitia ujasiri wake na ukakamavu katika huduma kwa umma.”

Katika mamlaka yake ya bunge, Bw Koinange aliungana na wengine ambao hivi majuzi walikuwa wamelenga kutunga sheria mpya za kuharamisha vuguvugu la Dkt Ruto la Hasla lakini kukazuka pingamizi kuu kutoka kwa hata kinara wa ODM Raila Odinga na washirika wake baada ya kuibuka kwamba ni mradi ungekuwa na madhara hasi kutoka kwa wapinzani wa Dkt Ruto.

Iliibuka kwamba sheria kama hiyo ingeonekana kama iliyolenga kuharamisha umasikini na ambayo ingezua mawimbi ya ukaidi miongoni mwa wengi nchini ambao kando na siasa, huishi maisha ya Uhasla.

Mauti ya Bw Koinange yanakuja wiki mbili tu baada ya aliyekuwa mbunge wa Kaunti jirani ya Juja Bw Francis Munyua Waititu kuaga dunia baada ya kuugua Kansa ya ubongo—haya yakiwa ni majonzi katika kaunti ya Kiambu yanayofuatana.

Kati ya 1968 na 1970 Bw Koinange alikuwa katika taasisi ya Tarkio nchini Marekani ambapo alijihami na taaluma ya Uzamili kuhusu masuala ya ujamii, Mazingira na siasa na kisha akahamia katika Jimbo la Ohio ambapo alizidisha masomo yake hadi uzamili wa Sheria za Kimataifa.

Mwaka wa 1972 alikuwa katika Wizara ya Spoti akiwa afisa wa nyanjani, kati ya 1974 na 1978 akiwa katika Wizara ya Leba akiwa naibu wa Katibu .

Mwaka wa hadi 1982 alikuwa katika Kampuni ya Mugawa Enteprises Ltd na Suncity Cinema Ltd akiwa Mkurugenzi, 1983 akiwa katika kampuni ya Video Tracts Revival, 1986 akiingia katika kazi ya ushauri katika safu za huduma za umma na za kibinafsi kabla ya kuchaguliwa kama mbunge wa Kiambaa mwaka wa 2013.

You can share this post!

TANZIA: Mbunge wa Kiambaa Paul Koinange afariki kutokana na...

Hii kafyu inaumiza wananchi – Kalonzo