KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Brazil kuvaana na Croatia kwenye robo-fainali

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Brazil kuvaana na Croatia kwenye robo-fainali

Na MASHIRIKA

BRAZIL walituma onyo kali kwa washiriki wengine wa Kombe la Dunia nchini Qatar mwaka huu kwa kutandika Korea Kusini 4-1 katika hatua ya 16-bora mnamo Jumatatu usiku ugani 974.

Mabao yote manne ya Brazil yalipachikwa wavuni katika kipindi cha kwanza kupitia kwa Vinicius Jr, Neymar Jr, Richarlson Andrade na Lucas Paqueta. Korea Kusini walifutiwa machozi na Paik Seung-ho kunako dakika ya 76.

Bao la Neymar lilikuwa lake la 76 akivalia jezi ya Brazil na sasa amesalia na goli moja pekee kufikia rekodi ya Pele ambaye ni mfungaji bora wa muda wote kambini mwa miamba hao.

Ushindi wa Brazil uliwakatia tiketi ya kukutana na Croatia katika pambano la robo-fainali mnamo Disemba 9, 2022 uwanjani Education City.

Chini ya kocha Adenor ‘Tite’ Bacchi, Brazil waliwapiga kumbo Uswisi kwa wingi wa mabao na kutawala Kundi G kwa alama sita, mbili mbele ya Cameroon na tano zaidi kuliko Serbia.

Wafalme hao mara tano wa dunia (1958, 1962, 1970, 1994, 2002) walianza kampeni za Kundi G kwa ushindi wa 2-0 dhidi ya Serbia kabla ya kulaza Uswisi 1-0 kisha kucharazwa 1-0 na Cameroon katika mechi iliyoshuhudia Tite akifanyia kikosi chake mabadiliko 10.

Kichapo hicho kutoka kwa Cameroon kilikomesha rekodi nzuri ya kutopigwa kwa Brazil katika michuano tisa mfululizo.

Brazil wamefuzu kwa raundi za muondoano kwenye Kombe la Dunia mara tisa mfululizo na miaka 32 imepita tangu Argentina iwapepete 1-0 na kuwabandua kwenye kivumbi hicho katika hatua ya 16-bora.

Kwa upande wao, Korea Kusini walipiku Uruguay kwa wingi wa mabao na kuambulia nafasi ya pili katika Kundi H baada ya kuokota pointi nne. Ureno walitawala kundi hilo kwa alama sita, tatu zaidi kuliko Ghana waliovuta mkia.

Wakitegemea zaidi maarifa ya Son Heung-min wa Tottenham Hotspur, Korea Kusini walifungua kampeni za Kundi H kwa sare tasa dhidi ya Uruguay kabla ya kukomoa Ghana 3-2 na kuangusha Ureno kwa mabao 2-1.

Kikosi hicho cha bara Asia kimewahi kusonga zaidi ya hatua ya 16-bora kwenye Kombe la Dunia mara moja pekee. Hiyo ilikuwa mwaka wa 2002 ambapo walitinga nusu-fainali. Hadi kufikia Jumatatu usiku, walikuwa wamekutana na Brazil mara ya mwisho mnamo Juni 2022 na wakakung’utwa 5-1 kirafiki.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Klabu ya Al-Nassr nchini Saudi Arabia yaweka mezani Sh25.8...

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Kocha Paulo Bento ajiuzulu baada...

T L