KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Cameroon wafunganya virago Qatar licha ya kushinda Brazil katika pambano la mwisho la Kundi G

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Cameroon wafunganya virago Qatar licha ya kushinda Brazil katika pambano la mwisho la Kundi G

Na MASHIRIKA

INGAWA Cameroon walikomoa Brazil 1-0 ugani Lusail Iconic katika pambano la mwisho la Kundi G kwenye fainali za Kombe la Dunia zinazoendelea nchini Qatar, mabingwa hao mara tano wa Afrika waliaga kipute hicho.

Fowadi Vincent Aboubakar alifungia Cameroon bao la pekee na la ushindi mwishoni mwa kipindi cha pili katika pambano hilo ila akaonyeshwa kadi ya pili ya manjano baada ya kuvua jezi akisherehekea.

Cameroon walianza mechi kwa matao ya juu na mshambuliaji Bryan akamwajibisha vilivyo kipa Ederson Moraes wa Manchester City aliyekuwa akichezeshwa na Brazil katika nafasi ya Alisson Becker wa Liverpool. Hata hivyo, ushindi wa 3-2 uliosajiliwa na Uswisi dhidi ya Serbia ulitosha kuzima ndoto ya Cameroon kuingia ndani ya raundi ya 16-bora.

Brazil waliojibwaga ugani dhidi ya Cameroon wakiwa tayari wamefuzu, walikifanyia kikosi chao cha kwanza mabadiliko 10. Fowadi matata wa Arsenal, Gabriel Martinelli, alipata fursa ya kudhihirisha ukubwa wa uwezo wake uwanjani ila makombora yake yakadhibitiwa na kupanguliwa na kipa Devis Epassy.

Licha ya kushindwa, Brazil walikamilisha kampeni zao za Kundi G kileleni na sasa watakutana na Korea Kusini katika mechi ya raundi ya 16-bora. Korea Kusini walifuzu baada ya kupepeta Ureno 2-1 na hivyo kuwapiga kumbo Uruguay waliocharaza Ghana 2-0 katika pambano jingine la Kundi H.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Uruguay waaga mashindano licha ya...

Waziri Namwamba atoa onyo kali baada ya Kenya kuondolewa...

T L