KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Ghana ndicho kikosi cha wanasoka wadogo zaidi kiumri katika Kombe la Dunia 2022

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Ghana ndicho kikosi cha wanasoka wadogo zaidi kiumri katika Kombe la Dunia 2022

Na CHRIS ADUNGO

KATI ya washiriki 32 wa Kombe la Dunia mwaka huu, Black Stars ya Ghana ndicho kikosi kinachojivunia wanasoka wa umri mdogo zaidi – wastani wa miaka 24.7 mbele ya Amerika (25.2), Ecuador (25.5) na Uhispania (25.6).

Mabingwa hao mara nne wa Kombe la Afrika (1963, 1965, 1978, 1982) walikosa kunogesha fainali za 2018 nchini Urusi baada ya kudenguliwa kwenye hatua ya makundi mnamo 2014 nchini Brazil.

Matokeo yao ya kuridhisha zaidi katika Kombe la Dunia ni 2010 ambapo Uruguay iliwang’oa kwa penalti 4-2 kwenye robo-fainali. Mwaka huu, wakijivunia kikosi ‘dhaifu zaidi’ katika kipindi cha miaka 15 iliyopita, wametiwa katika Kundi H pamoja na Ureno, Korea Kusini na wafalme mara mbili wa dunia, Uruguay.

Miongoni mwa chipukizi watakaobeba matumaini finyu ya kikosi hicho cha kocha Otto Addo nchini Qatar ni Tariq Kwame Nii-Lante Lamptey. Beki huyo wa kupanda na kushuka mwenye umri wa miaka 22 sasa anachezea Brighton ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Baada ya kuwakilisha Uingereza katika umri mdogo akivalia jezi za chipukizi wasiozidi umri wa miaka 18 na 21, Lamptey alibadilisha uraia na akasakatia Ghana mara ya kwanza mnamo Septemba 2022. Alitokea benchi katika kipindi cha pili kwenye mechi ya kirafiki iliyoshuhudia Ghana wakipepetwa na Brazil 3-0 mjini Le Harve, Ufaransa.

Alizaliwa katika eneo la Hillingdon jijini London na akachezea Larkspur Rovers kabla ya kusajiliwa na akademia ya Chelsea akiwa na umri wa miaka minane.

Mechi yake ya kwanza kambini mwa Chelsea ilikuwa dhidi ya Arsenal mnamo Disemba 29, 2019 ambapo alitokea benchi kujaza nafasi ya Fikayo Tomori. Alisaidia waajiri wake kutoka nyuma kwa 1-0 na kusajili ushindi wa 2-1. Aliondoka ugani Stamford Bridge mnamo Januari 2020 na akatia saini mkataba wa miaka mitatu na nusu kambini mwa Brighton.

Mnamo 2010, Ghana walibanduliwa na Uruguay kupitia penalti baada ya kuambulia sare ya 1-1 chini ya dakika 120. Mshindi wa mechi hiyo aliamuliwa kupitia matuta fowadi Asamoah Gyan alipopoteza penalti mwishoni mwa muda wa ziada baada ya Luiz Suarez kunawa mpira ndani ya kijisanduku na kuonyeshwa kadi nyekundu.

“Itakuwa fursa nzuri ya kulipiza kisasi dhidi ya Uruguay. Tulikuwa tumewashinda mnamo 2010 katika hatua muhimu lakini Suarez akatunyima nafasi ya kuandikisha historia. Tukio hilo, ambalo lingali bichi akilini mwetu, litatuchochea kuwazamisha,” akasema rais wa Shirikisho la Soka la Ghana, Kurt Okraku.

Suarez, 35, sasa anasakatia kikosi cha Nacional nchini Uruguay na amewahi pia kuvalia jezi za Liverpool, Barcelona na Atletico Madrid. Huku akiwa bado sehemu ya kikosi kitakachotegemewa na Uruguay nchini Qatar, Ghana haitakuwa na mchezaji yeyote aliyeunga timu yao miaka 12 iliyopita.

Hii ni mara ya tano kwa Ghana wanaoshikilia nafasi ya 61 kimataifa kushiriki Kombe la Dunia. Ni mataifa matatu pekee kutoka Afrika ambayo yamewahi kutinga robo-fainali za Kombe la Dunia – Cameroon (1990), Senegal (2002) na Ghana (2010).

KIKOSI CHA GHANA:

MAKIPA:  Lawrence Ati-Zigi (St Gallen), Abdul Manaf Nurudeen (Eupen), Ibrahim Danlad (Asante Kotoko)

MABEKI: Daniel Amartey (Leicester), Abdul-Rahman Baba (Reading), Alexander Djiku (Strasbourg), Joseph Aidoo (Celta Vigo), Gideon Mensah (Bordeaux), Denis Odoi (Club Brugge), Tariq Lamptey (Brighton), Alidu Seidu (Clermont), Mohammed Salisu (Southampton)

VIUNGO: Mohammed Kudus (Ajax), Thomas Partey (Arsenal), Andre Ayew (Al Saad), Elisha Owusu (Gent), Daniel-Kofi Kyereh (St Pauli), Daniel Afriyie Barnieh (Hearts of Oak), Salis Abdul Samed (Lens)

WAVAMIZI: Antoine Semenyo (Bristol City), Abdul Fatawu Issahaku (Sporting CP), Jordan Ayew (Crystal Palace), Kamaldeen Sulemana (Rennes), Osman Bukari (Red Star Belgrade), Felix Afena-Gyan (Roma), Inaki Williams (Athletic Bilbao), Kamal Sowah (Club Brugge).

You can share this post!

TAHARIRI: Usalama uanze na wewe Kombe la Dunia likianza

Man-United kutamatisha mkataba wa Ronaldo kisheria ili...

T L