KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Kocha Paulo Bento ajiuzulu baada ya kikosi chake cha Korea Kusini kudenguliwa katika raundi ya 16-bora

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Kocha Paulo Bento ajiuzulu baada ya kikosi chake cha Korea Kusini kudenguliwa katika raundi ya 16-bora

Na MASHIRIKA

KOCHA wa Korea Kusini, Paulo Bento, alijiuzulu baada ya kikosi chake kudenguliwa katika hatua ya 16-bora kwenye fainali za Kombe la Dunia zinazoendelea nchini Qatar.

Korea Kusini waling’olewa na Brazil baada ya kupokezwa kichapo cha 4-1 mnamo Disemba 5, 2022 ugani 974. Ushindi huo wa Brazil ambao ni mabingwa mara tano wa dunia uliwakatia tiketi ya kumenyana na Croatia katika hatua ya robo-fainali.

Croatia waliopigwa 4-2 na Ufaransa katika fainali ya 2018 nchini Urusi, walifuzu kwa robo-fainali za mwaka huu baada ya kufunga Japan penalti 3-1 baada ya kutoshana nguvu kwa sare ya 1-1 katika muda wa kawaida.

Bento, 53, ni raia wa Ureno aliyepokezwa mikoba ya Korea Kusini mnamo Agosti 2018.

“Lazima nianze kufikiria kuhusu mustakabali wangu kitaaluma. Na bila shaka sitakuwa tena kocha wa Korea Kusini,” akatanguliza Bento.

“Nishatangazia wachezaji msimamo wangu na kumweleza pia rais wa Shirikisho la Soka la Korea Kusini kuhusu maamuzi hayo ambayo niliyafanya Septemba 2022,” akaongezea.

Chini ya Bento, Korea Kusini walipiku Uruguay kwa wingi wa mabao na kuambulia nafasi ya pili katika Kundi H baada ya kuokota pointi nne nchini Qatar. Ureno walitawala kundi hilo kwa alama sita, tatu zaidi kuliko Ghana waliovuta mkia.

Wakitegemea zaidi maarifa ya Son Heung-min wa Tottenham Hotspur, Korea Kusini walifungua kampeni za Kundi H kwa sare tasa dhidi ya Uruguay kabla ya kukomoa Ghana 3-2 na kuangusha Ureno kwa mabao 2-1.

Kikosi hicho cha bara Asia kimewahi kusonga zaidi ya hatua ya 16-bora kwenye Kombe la Dunia mara moja pekee. Hiyo ilikuwa mwaka wa 2002 ambapo walitinga nusu-fainali. Waliwahi tena kukutana na Brazil mnamo Juni 2022 na wakakung’utwa 5-1 kirafiki.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Brazil kuvaana na Croatia kwenye...

Kampuni ya bima, Aga Khan kutoa matibabu ya bure

T L