KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Nyota Breel Embolo aongoza Uswisi kuzamisha chombo cha Cameroon katika Kundi G

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Nyota Breel Embolo aongoza Uswisi kuzamisha chombo cha Cameroon katika Kundi G

Na MASHIRIKA

FOWADI Breel Embolo alifunga bao la pekee katika ushindi wa 1-0 uliosajiliwa na timu yake taifa ya Uswisi dhidi ya Cameroon katika pambano la ufunguzi wa Kundi G kwenye fainali za Kombe la Dunia nchini Qatar.

Hata hivyo, nyota huyo anayechezea AS Monaco ya Ufaransa, hakusherehekea bao hilo ikizingatiwa kwamba Cameroon ndiko alikozaliwa na kulelewa.

Licha ya kuanza mechi kwa matao ya juu, Indomitable Lions wa Cameroon walipoteza nafasi nyingi za wazi katika pambano hilo lililosakatiwa ugani Al Janoub.

Ushindi huo ulikuwa muhimu zaidi kwa Uswisi ambao sawa na Cameroon, bado wana kibarua kizito dhidi ya Brazil – mabingwa mara tano wa dunia wanaopigiwa upatu wa kunyanyua taji la mwaka huu nchini Qatar.

Embolo alipata uraia wa Uswisi mnamo 2014 baada ya familia yake kuondoka Cameroon na kuhamia katika taifa hilo akiwa na umri wa miaka sita.

Akiwa na umri wa miaka 18, alianzisha Wakfu wa Embolo kwa lengo la kusaidia watoto wakimbizi nchini Uswisi pamoja na watoto maskini katika taifa la Cameroon alikozaliwa.

Kabla ya kuongoza Uswisi kushuka dimbani dhidi ya Cameroon, alisema alihisi tukio hilo kuwa “spesheli mno” na alipofunga bao, alinyanyua mikono yake na kufumba macho.

“Nilimwambia Breel kuwa Cameroon ni marafiki zako tu hadi kipenga cha kuashiria mwanzo wa mechi kitakapopulizwa. Baada ya hapo, watakuwa wapinzani ambao lazima tuwaangushe,” akasema kocha Murat Yakin.

Mkufunzi wa Cameroon, Rigobert Song alisema “angependa sana Embolo awe upande wa kikosi chake” huku akisisitiza kwamba anamstahi na kumuonea fahari kubwa nyota huyo mwenye umri wa miaka 25.

Nahodha wa Uswisi ambaye ni kiungo wa Arsenal, Granit Xhaka alisema ushindi dhidi ya Cameroon unawapa motisha kubwa ya kulaza Serbia na Brazil katika michuano miwili ijayo ya Kundi G na kufuzu kwa hatua ya 16-bora.

Cameroon sasa wamepoteza mechi nane mfululizo kwenye fainali za Kombe la Dunia. Sasa wana ulazima wa kupepeta Serbia katika pambano lijalo mnamo Novemba 28, 2022 ili kuweka hai matumaini ya kusonga mbele zaidi ya hatua ya makundi kwa mara ya kwanza tangu 1990. Uswisi watavaana na Brazil mnamo Novemba 28, 2022 ugani 974 Stadium.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Ronaldo aweka rekodi mpya ya...

Muuzaji nyama atozwa faini ya Sh1,000 au jela siku 14 kwa...

T L