KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Uholanzi na Ecuador nguvu sawa katika Kundi A nyota Enner Valencia akifikisha mabao matatu kibindoni

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Uholanzi na Ecuador nguvu sawa katika Kundi A nyota Enner Valencia akifikisha mabao matatu kibindoni

Na MASHIRIKA

ENNER Valancia alifunga bao lake la tatu kwenye fainali za Kombe la Dunia mwaka huu kabla ya kuondolewa uwanjani kwa machela katika pambano la Kundi A lililokamilika kwa sare ya 1-1 dhidi ya Uholanzi ugani Khalifa International.

Fowadi matata wa PSV Eindhoven, Cody Gakpo, aliwaweka Uholanzi kifua mbele baada ya dakika tano na sekunde nne za mchezo – bao lake lilikuwa la haraka zaidi kufikia sasa kwenye fainali za Kombe la Dunia nchini Qatar.

Hata hivyo, Ecuador walijituma maradufu na wakasawazisha mambo mwanzoni mwa kipindi cha pili baada ya bao walilofunga kupitia kwa Pervis Estupinan mwishoni mwa kipindi cha kwanza kutohesabiwa. Ecuador nusura wafunge bao la pili kupitia kwa Gonzalo Plata kunako dakika ya 52.

Nahodha Valencia, aliyefunga mabao yote mawili ya Ecuador katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Qatar kwenye mchuano wa ufunguzi wa fainali za mwaka huu mnamo Novemba 20, 2021, alitatiza sana mabeki wa Uholanzi.

Nyota huyo wa zamani wa West Ham United na Everton hata hivyo alizidiwa na maumivu mwishoni mwa kipindi cha pili na akaondolewa uwanjani kwa machela.

Matokeo kati ya Uholanzi na Ecuador yanaacha wazi Kundi A kwa vikosi vitatu sasa kuwania nafasi ya kutinga hatua ya 16-bora baada ya Qatar waliopokezwa kichapo cha 3-1 na Senegal kudenguliwa.

Huku Uholanzi wakipigiwa upatu wa kuzamisha Qatar katika pambano la mwisho la Kundi A, macho yote sasa yataelekezwa kwa gozi kali la kufa-kupona litakalokutanisha Ecuador na Senegal.

Bao la Gakpo lilikuwa la kwanza la Ecuador kufungwa baada ya dakika 701 za mchezo katika mapambano yote na la kwanza tangu Machi 2022.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Richarlson aongoza Brazil...

Vinara wakuu Azimio washutumu Kenya Kwanza kwa kulipiza...

T L