Habari MsetoSiasa

Komeni kulalamika kuhusu ushuru, Ruto awaambia Wakenya

September 25th, 2018 2 min read

WYCLIFFE KIPSANG NA LEONARD ONYANGO

NAIBU Rais William Ruto ametetea hatua ya serikali kuongeza ushuru akiwataka Wakenya ‘kutopiga kelele’.

Bw Ruto alisema nyongeza hiyo ya ushuru itawezesha serikali kupata fedha zaidi za kuendeshea miradi ya maendeleo.

Alisema serikali haitafuja fedha zitakazokusanywa na ushuru utakaokusanywa.

Hatua ya serikali kuongeza ushuru imeshutumiwa vikali na Wakenya kwani unawaongezea gharama ya maisha.

Mswada wa kuongeza ushuru uliungwa mkono na Rais Uhuru Kenyatta, kinara wa ODM Raila Odinga na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka.

“Uchumi wa nchi hii hautastawi ikiwa tutaendelea na malumbano. Kila Mkenya ajiandae kulipa ushuru ili nchi ipate raslimali za kutosha kwa ajili ya maendeleo,” akasema Bw Ruto aliyekuwa akizungumza mjini Kapsabet wakati wa uzinduzi wa Miradi Minne ambayo serikali ya Kaunti ya Nandi inalenga kutekeleza katika kipindi cha miaka minne ijayo.

Naibu Rais alisema fedha zinazokopwa na serikali kutoka mataifa ya ughaibuni zimekuwa zikitumiwa kulipa madeni.

Tangu serikali ya Jubilee kuingia mamlakani mnamo 2013, deni limeongezeka maradufu kutoka Sh2 trilioni hadi Sh5 trilioni. Hiyo inamaanisha kuwa kila Mkenya anadaiwa Sh100,000.

Bw Ruto, hata hivyo, alionya wafanyabiashara walaghai wanaopunja Wakenya kwa kuongeza bei ya bidhaa maradufu kutokana na kisingizio cha kuongezeka kwa ushuru wa mafuta.

“Ikiwa nauli ya gari ilikuwa Sh100 hiyo inamanisha kuwa nauli imeongezeka hadi Sh108. Lakini jambo la kushangaza ni kwamba baadhi ya wamiliki wa magari ya usafiri wa umma wameongeza nauli hadi Sh200. Tushirikiane tung’oe wafanyabiashara hawa walaghai,” akasema.

Bw Ruto.

“Inasikitisha kuona wafanyabiashara wa vichinjio wakiongeza bei ya nyama kutokana na kisingizio kwamba ushuru wa mafuta umeongezwa. Kwani ng’ombe wanakunywa petroli?” akaongezea.

Bw Ruto, vilevile, alitetea ushuru wa wa asilimia 1.5 unaotozwa katika mishahara ya wafanyakazi huku akisema kuwa fedha hizo zitakusanywa katika hazina moja ili kuwajengea Wakenya maskini nyumba.

Hata hivyo, seneta wa Makueni Mutula Kilonzo Jr ambaye pia alihudhuria hafla hiyo ya uzinduzi alitofautiana vikali na Bw Ruto kuhusu ushuru huo wa nyumba.

“Ukweli usemwe, Wakenya wanaumizwa na ushuru hivyo tutataka serikali ifutilie mbali ushuru huyo wa nyumba, haufai,” akasema Bw Kilonzo.