Habari Mseto

Konchellah apoteza kiti chake

August 1st, 2018 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MBUNGE wa Kilgoris Bw Gideon Konchellah alipoteza kiti baada ya Mahakama ya rufaa kufutilia mbali ushindi wake Jumanne.

Majaji Milton Makhandia, Daniel Musinga na Gatembu Kairu walikubaliana na aliyekuwa wakati mmoja waziri wa masuala ya usalama Bw Julius ole Sunkuli kwamba kulikuwa na kasoro tele katika zoezi la kuhesabu kura.

Majaji hao walisema kulikuwa na ushahidi wa kutosha kwamba kura zilibadilishwa katika vituo viwili na maafisa waliosimamia uchaguzi.

Majaji  Makhandia, Musinga na Kairu  walimkosoa Jaji Martin Muya aliyesikiza kesi hiyo kwa kupuuza madai kwamba matokeo katika kiituo cha kupigia kura cha shule ya msingi cha Enenkeshui yalibadilishwa na Bw Onyinkwa Obara almaarufu Leparan Jacob.

Majaji hao walisema jambo hilo lilikuwa mbaya na liliathiri matokeo,

Bw  Konchellah alitangazwa mshindi baada ya kuzoa kura 23,812 naye Bw Sunkuli akawai kura 17,160.

Bw Sunkuli aliyekuwa balozi wa Kenya nchini Uchina alidai kura ziliborongwa katika vituo 100.

Tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC ilikiri kulikuwa na kasoro katika matokeo ambayo hayangeweza kuepukika.