Habari Mseto

Kondakta afa kwa kudungwa kisu na mkewe

June 2nd, 2024 1 min read

NA WYCLIFFE NYABERI

POLISI mjini Kisii wanamzuilia mwanamke mmoja anayedaiwa kumuua mumewe kwa kumchoma kisu.

Tukio hilo la Alhamisi, Mei 30 katika soko la Ibeno, eneobunge la Nyaribari Chache limeacha majirani na mshtuko.

Kulingana na ripoti ya polisi, kulitokea mabishano baina ya Wesley Aringa, 28, na mkewe mwenye umri wa miaka 22, mida ya saa tatu za usiku za siku hiyo.

Kufuatia malumbano kati ya wawili hao, mke huyo anasemekana kuchukua kisu cha jikoni na kumchoma mumewe kifuani.

Marehemu Aringa alianza kuvuja damu nyingi na alifungua mlango wa chumba chao cha kukodisha kwenda kutafuta usaidizi.

Lakini kwa bahati mbaya, alilemewa na kuanguka mita chache nje ya mlango wa chumba chake na kufariki.

Marehemu Aringa alikuwa kondakta wa matatu mjini Kisii.

Mshukiwa wa kifo hicho alinaswa na maafisa wa polisi huku uchunguzi ukianzishwa mara moja.

“Kisu cha jikoni kilichokuwa na matone ya damu kilipatikana nyumbani kwao. Mshukiwa huyo alikamatwa na anasaidia katika uchunguzi,” ilisema sehemu ya ripoti ya polisi ambayo Taifa Leo ilifanikiwa kuiona.

Mwili wa mwendazake ulipelekwa katika hifadhi ya maiti ya Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Kisii (KTRH) kusubiri upasuaji.