KONGAMANO LA CHAKAMA: Kongamano laanza leo Alhamisi katika Chuo Kikuu cha Maasai Mara

KONGAMANO LA CHAKAMA: Kongamano laanza leo Alhamisi katika Chuo Kikuu cha Maasai Mara

Na CHRIS ADUNGO

KONGAMANO la Kimataifa la Chama cha Kiswahili Afrika Mashariki (CHAKAMA) litafunguliwa leo Alhamisi na Gavana wa Kaunti ya Narok, Mheshimiwa Samuel Kuntai Ole Tunai katika Chuo Kikuu cha Maasai Mara, Narok.

Kongamano la CHAKAMA ambalo huandaliwa kila baada ya miaka miwili, ndilo maarufu zaidi miongoni mwa wasomi, wataalamu, wapenzi wa Kiswahili na wahadhiri wa vyuo vikuu kutoka ndani na nje ya Afrika Mashariki.

Ingawa mada kuu ya kongamano la mwaka huu ni ‘Kiswahili na Lugha nyingine za Kiafrika katika Maendeleo ya Jamii’, zaidi ya wajumbe 100 watakaoshiriki watapania pia kulinganisha mitazamo ya matumizi ya Kiswahili katika nyanja mbalimbali ili kujadiliana na kuweka wazi mikakati ya kuiendeleza lugha hii ashirafu katika eneo zima la Afrika Mashariki na ulimwengu kwa jumla.

Wajumbe wataazimia pia kutathmini Nafasi ya Kiswahili katika Ustawi wa Jinsia na Uana na kujadili Nafasi ya Kiswahili katika Utalii tangu Kiswahili kitambuliwe kuwa Lugha Rasmi ya Kenya kwa mujibu wa Katiba Mpya ya 2010.

Kulingana na Dkt James Ontieri ambaye ni Mwenyekiti wa CHAKAMA na Mhadhiri wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Maasai Mara, washiriki wa kongamano hili la siku mbili watalenga pia kujadili nafasi ya Kiswahili katika ulimwengu wa sasa na haja ya Waswahili wenyewe kuhakikisha kuwa hawawi nyuma katika kuijengea lugha hii muhimu nafasi maridhawa kwenye majukwaa mbalimbali ya kimataifa.

Kongamano litahudhuriwa na idadi kubwa ya wajumbe kutoka Kenya, Tanzania, Uganda na Rwanda. Baadhi ya wageni kutoka mataifa ya nje na sehemu nyinginezo za humu nchini walianza kuwasili katika Chuo Kikuu cha Maasai Mara mnamo Jumanne.

Dkt Mussa Hans ambaye kwa sasa ni Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI) anaongoza kundi la wajumbe kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Tanzania huku Profesa Pacifique Malonga akiwa kati ya washiriki watakaowakilisha taifa la Rwanda.

Kongamano litanogeshwa na uwepo wa Dkt Jagero Akinyi (Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Jaramogi Oginga Odinga), Dkt Joseph Nyehita Maitaria (Chuo Kikuu cha Karatina), Dkt Hannah Mwaliwa Chaga (Chuo Kikuu cha Nairobi), Dkt Silas Owala (Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Jaramogi Oginga Odinga), Dkt Alexander Rotich (Chuo Kikuu cha Kabianga), Bw Francis Waititu (Chuo Kikuu cha Moi) na Katibu Mkuu Mtendaji wa Kamisheni ya Kiswahili Afrika Mashariki (KAKAMA), Profesa Kenneth Inyani Simala.

Kundi la wajumbe kutoka Uganda litakuwa chini ya usimamizi na uelekezi wa Dkt Idah Mutenyo wa Chuo Kikuu cha Kabale, Dkt Caroline Asiimwe wa Chuo Kikuu cha Makerere na Dkt Levi Masereka. Dkt Mutenyo ambaye kwa sasa ni Naibu Mwenyekiti wa CHAKAMA anatazamiwa kupokezwa rasmi mikoba ya uenyekiti wa chama katika kongamano la mwaka 2019.

Kamati Tendaji ya CHAKAMA kwa sasa ipo chini ya uongozi wa Dkt Ontieri (Mwenyekiti), Dkt Leonard Chacha (Katibu), Dkt Asiimwe (Naibu Katibu Mkuu), Dkt Mwaliwa (Mwekahazina), Dkt Shadidu Ndossa (Afisa Mwenezi), Dkt Zainab Iddi (Afisa wa Ushirikiano) na Dkt Mark Mosol Kandagor (Mhariri Mkuu).

Dkt Ndossa na Dkt Iddi ni miongoni mwa washiriki kutoka Tanzania ambao kufikia sasa wamethibitisha kuhudhuria kongamano hili. Dkt Mwahija wa State University of Zanzibar (SUZA) atawakilisha Zanzibar.

Naibu Makamu Mkuu wa Masuala ya Wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Moi, Profesa Nathan Oyori Ogechi atawasilisha Makala Elekezi ya kongamano.

Upekee

Akizungumza na Taifa Leo mnamo Jumanne, Dkt Ontieri alifichua baadhi ya mambo ambayo kulingana naye, yatalifanya kongamano la CHAKAMA mwaka huu kuwa na upekee zaidi.

“Litawaleta pamoja wakufunzi wa Kiswahili, watafiti, wanafunzi, wanahabari, wasanii, wanaharakati, wanafasihi, wachapishaji, wawakilishi kutoka Serikali ya Kaunti ya Narok, wakereketwa na wadau wa Kiswahili kutoka janibu mbalimbali za Afrika Mashariki” akasema kwa kusisitiza kuwa kongamano litahudhuriwa pia na wanachama 27 wa Chama cha Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Maasai Mara (CHAKIMMA) kwa niaba ya Chama cha Wanafunzi wa Kiswahili katika Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki (CHAWAKAMA).

Ni katika kongamano hili ambapo viongozi wapya wa CHAKAMA watachaguliwa na pia kitabu chenye baadhi ya makala yaliyowasilishwa na washiriki katika makongamano ya awali kuzinduliwa.

“Wingi wa makala zilizowasilishwa katika makongamano ya awali ya CHAKAMA jijini Dodoma, Tanzania (2017) na katika Chuo Kikuu cha Mount Kenya mjini Thika (2015) ulizalisha machapisho ambayo yatazinduliwa katika kongamano litakaloandaliwa jijini Kampala, Uganda mnamo 2021. Hadi Chuo Kikuu cha St Augustine, Tanzania kilipokuwa mwenyeji wa kongamano la CHAKAMA mnamo 2013, makongamano mengine ya chama yalikuwa yameandaliwa jijini Kampala na katika Bontana Hotel mjini Nakuru, Kenya mnamo 2009 na 2011 mtawalia.

Dkt Ontieri anatambua upekee wa mchango wa Chuo Kikuu cha Maasai Mara chini ya uongozi wa Kaimu Makamu Mkuu, Profesa Kitchie Magak na Naibu Makamu Mkuu wa Akademia na Masuala ya Wanafunzi, Profesa Bulitia katika kufanikisha mchakato na shughuli za maandalizi ya kongamano la CHAKAMA mwaka 2019.

“Waandalizi mpaka sasa wamejitahidi sana na wanaendelea kujituma ipasavyo. Tumepanga mambo mengi makubwa humu chuoni. Ukumbi umepambwa vilivyo tayari kumeza na hata kuwatema baadhi ya wajumbe watakaohudhuria Kongamano la CHAKAMA 2019,” akasema Dkt Ontieri.

Kongamano litafungwa rasmi na Naibu Makamu Mkuu wa Masuala ya Utawala, Fedha na Mipango katika Chuo Kikuu cha Maasai Mara, Prof Abdille hapo kesho na washiriki kupata fursa ya kutembelea Mbuga ya wanyama pori ya Maasai Mara.

Mbali na Serikali ya Kaunti ya Narok, wadau wengine ambao wamefanikisha maandalizi ya kongamano la CHAKAMA mwaka 2019 kwa namna moja au nyingine ni, kampuni ya Nation Media Group (NMG), Oxford University Press (OUP), Longhorn Publishers, East African Educational Publishers (EAEP), Kenya Broadcasting Corporation (KBC), Glenmark Pharmaceuticals Ltd na Ewaso Ngiro South Development Authority (ENSDA).

You can share this post!

Magoha awataka wazazi Migori waache kulialia baada ya eneo...

AKILIMALI: Mpishi hodari akiri ufugaji wa ng’ombe...

adminleo