Habari Mseto

Kongamano la kimataifa kuanza huku viongozi wa kidini wakihofia maovu

November 9th, 2019 2 min read

Na MARY WANGARI

KONGAMANO la Kimataifa kuhusu Idadi ya Watu na Maendeleo (ICPD) limetangaza maudhui matano muhimu yatakayoangaziwa katika warsha hiyo ya kuadhimisha miaka 25 itakayoandaliwa Nairobi, wiki ijayo, huku likikabiliwa na pingamizi kali kutoka kwa viongozi wa kidini nchini.

Kulingana na taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti yake, ajenda kuu zitakazotiliwa maanani katika kongamano hilo ni pamoja na: uwezo wa kupata haki na huduma za uzazi kama sehemu ya huduma ya afya duniani, ufadhilli unaohitajika kukamilisha Mradi wa Utekelezaji wa ICPD na kustawisha yaliyofanikishwa, jinsi ya kutumia tofauti za kimaeneo kuendesha ukuaji wa uchumi na kufanikisha ustawishaji wa maendeleo.

Kukomesha dhuluma za kijinsia na mila mbovu pamoja na kuunga mkono haki za kupata huduma ya afya ya uzazi hata katika hali ya kibinadamu na dhaifu, ni miongoni mwa ajenda zitakazoangaziwa vilevile, katika kongamano hilo la siku tatu kuanzia Jumanne, Novemba 12 hadi Alhamisi Novemba 14.

Kongamano hilo linahusisha viongozi wa mataifa 179, waliobuni Mradi wa Utekelezaji uliolenga kuimarisha haki za wanawake na wasichana, kwa maslahi yao binafsi, familia zao, jamii na mataifa kwa jumla, taarifa hiyo ilisema.

“Kongamano la Nairobi litaimarisha jamii ya kimataifa, kufufua upya ajenda ya ICPD, kustawisha na kuchochea manufaa yaliyofanikishwa tangu 1994. Litakuwa jukwaa kwa serikali na mashirika mengine kutangaza kwa hiari malengo kimataifa, ikiwemo ya kifedha, yatakayoharakisha maendeleo,”ilisema taarifa hiyo.

Kulingana na shirika hilo ambalo mojawapo wa wafadhili wake wakuu ni Ubalozi wa Denmark nchini Kenya na Uganda, mifumo ya kiubunifu kuhusu fedha na rasilimali nyinginezo kutoka serikali, mashirika ya kifedha kimataifa na taasisi za kibinafsi, itahitajika ili kufanikisha malengo ya ICPD kufikia 2030.

Hata hivyo, kongamano hili limejiri huku likikabiliwa na pingamizi kuu kutoka kwa viongozi wa kidini nchini wanaoshuku warsha hiyo ina nia fiche.

Viongozi hao wanaojumuisha asasi zote za kidini ikiwemo Wakristo, Waislamu na Wahindu, wanadai kuwa ajenda kadha zinazotazamiwa kupitishwa katika kongamano hilo, zinahusu kuendeleza ushoga, uavyaji mimba na matendo mengine maovu.