Habari

Kongamano la kuwaleta pamoja wanaume pekee laendelea mjini Eldoret

October 21st, 2019 1 min read

Na MWANDISHI WETU

KONGAMANO la kwanza na la aina yake linalohusisha wanaume pekee linaandaliwa katika hoteli ya Nobel mjini Eldoret.

Miongoni mwa watu wenye umaarufu mkubwa wanaohudhuria kongamano hilo kwa jina Eldoret City Men Congress ni Jackson Kibor na Profesa Lukoye Atwoli miongoni mwa watu wengine.

Taifa Leo inafuatilia yatakayojadiliwa na bila shaka itakufahamisha msomaji.

Kwa wengi, Kibor si mgeni kwao. Kwa miaka kadha amekuwa akitajwa kwa sababu ya patashika ya hapa na pale inayohusu migogoro katika maisha yake ya ndoa.

Mwaka 2018 kulikuwa na kesi mahakamani akitalikiana na mkewe ambaye alikuwa ameishi naye kwa miaka 52.

Pia amewahi kulumbana na wanawe shambani na pia mahakamani huku kando yake akiwa na kidosho ambaye alisema anamfahamu kama mke halali.

Zamani akiwa afisa wa polisi, Kibor ni mkulima na mfugaji tajiri ambaye ana umri wa miaka 85 kwa sasa.

Kuhusu kuomba talaka, Kibor alikimbia mahakamani mwaka wa 2014 akidai kuwa mkewe, Bi Josephine Jepkoech Kibor, alikuwa amegeuka kuwa kinyume na penzi lililowaleta pamoja na kwa wakati huo alikuwa ametoweka nyumbani na kumtesa.

Katika mahakama ya Eldoret, Hakimu Mwandamizi, Charles Obulutsa alikubaliana na Kibor kuwa maisha yake yangeweza tu kupata utulivu iwapo wangetenganishwa kisheria.