Jamvi La Siasa

Kongamano la Limuru III laendelea kuibua hisia zikisalia saa chache

May 16th, 2024 3 min read

NA MWANGI MUIRURI

HUKU baadhi ya wadau wa siasa na utamaduni wa Mlima Kenya wakijiandaa kufika katika kongamano la Limuru III kujadili masilahi ya wenyeji katika utawala wa serikali ya Rais William Ruto, vijana wametoa kauli zao.

Mwandalizi mkuu wa Limuru III ni aliyekuwa mgombea mwenza wa Raila Odinga katika uchaguzi wa urais mwaka 2022 Bi Martha Karua, akisaidiana na wandani wa Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta.

Ni mpango unaoungwa mkono na Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni, aliyekuwa Gavana wa Meru Peter Munya, aliyekuwa Gavana wa Murang’a Bw Mwangi wa Iria, aliyekuwa kinara wa kundi haramu la Mungiki Bw Maina Njenga, aliyekuwa Waziri wa Afya Mutahi Kagwe, aliyekuwa Gavana wa Laikipia Bw Ndiritu Muriithi pamoja na Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Agikuyu Bw Wachira Kiago.

Ni kongamano ambalo limepandisha hisia za kisiasa eneo la Mlima Kenya huku walio na imani kwa utawala wa Rais Ruto wakidai kwamba nia kuu ya waandalizi ni kudunisha serikali nao walio katika mtazamo mbadala wakishikilia kwamba linafaa.

Katika hali hizo, tuliwasaka wawili katika mirengo hiyo ambao ni aliyekuwa Waziri Msaidizi wa Michezo Zack Kinuthia na mwenyekiti wa kitaifa wa kongamano la vijana wa Democratic Congress Bi Gladys Njoroge.

Aliyekuwa Waziri Msaidizi wa Michezo Zack Kinuthia (kulia) na mwenyekiti wa kitaifa wa kongamano la vijana wa Democratic Congress Bi Gladys Njoroge. PICHA | MAKTABA

Bw Kinuthia huwa anajihusisha na siasa zilizo na imani kwa rais mstaafu Uhuru Kenyatta huku naye Bi Njoroge akisisitiza kwamba mirengo yote ya kisiasa eneo la Mlima Kenya ni halali, kile kinachohitajika tu ni nia njema katika kila mikakati.

“Wote katika mirengo yote ni wetu ima wawe wabaya au wazuri. Wote ni sisi na sisi ni wao, hivyo cha maana ni kusaka ule mstari wa kuungama katika masilahi ya eneo lakini sio ya kibinafsi. Kwa sasa hili kongamano liko na ubinafsi mwingi,” akadai Bi Njoroge.

Bw Kinuthia anasema kwamba kongamano la Limuru III linafaa.

“Tunataka kujieleza sisi watu wa Mlima Kenya kwamba tulihadaiwa tukaweka kura kwa kapu ambalo limegeuka kuwa la kuitisha ushuru wa juu,” akasema Bw Kinuthia.

Alisema kwamba kongamano hilo ni la kuteta kwamba mambo yakiendelea jinsi yalivyo, ushuru utaendelea kutozwa huku mwingine ukiletwa bila hata kuzingatia hesabu za faida au hasara.

Katika hali hiyo, Bw Kinuthia alisema kwamba “ni vyema tujitokeze kama wadau wa Mlima Kenya tuonyeshe waziwazi kwamba tumekataa kukandamizwa kwa kiwango hicho cha kumaliziwa sekta zetu za kiuchumi”.

Aidha, alisena kwamba kila wakati watu wa Mlima Kenya wakisema wanaamka kukutana, huwa ni shida kwa wale walio katika uongozi lakini jamii nyingine zikikutana, zinasemwa kwamba zinasaka uzalendo wa kijamii na kitaifa.

Bw Kinuthia aliutaka utawala wa Rais Ruto na Naibu Rais Rigathi Gachagua ujue kwamba wakati umewadia wa kuelezewa ukweli halisi kuhusu hali katika Mlima Kenya na pia kuhusu mbinu za kujikomboa ifikapo 2027.

“Ni lazima tuwaambie hata ikiwa hawataki kuambiwa kwamba Mlima Kenya tunataka bei za mazao shambani ziimarike, tupewe rasilimali za kitaifa kwa kigezo cha wingi wetu, ushuru upunguzwe, maeneobunge ya kwetu yakadiriwe mipaka upya na kwamba tunaunda chama chetu cha kujikomboa 2027 na 2032,” alisema.

Bi Njoroge alisema kwamba kongamano hilo la Limuru III linafaa lakini lipangwe kwa njia za uwazi, wadau wote muhimu wahusishwe na lisiwe ni la kupiga kelele na kisha kuelekea nyumbani pasipo afueni kwa mpigakura wa kawaida wa eneo hilo.

“Hakuna shida ya jamii kukutana. Hata tunafaa, ikiwezekana, kukutana mara tatu kwa siku ndio tupange mambo yetu, tuyajadili, tuelewane na tusonge mbele kwa njia ya uwiano. Shida iliyoko kwa sasa ni kwamba waliopanga Limuru III wako na njama fiche ya kujipigia debe kisiasa,” akasema.

Alisema kwamba “kongamano halisi ambalo linaweza likasaidia Mlima Kenya linafaa kwanza lianze pembeni ambapo wadau muhimu watatoa mapendekezo na yawasilishiwe wenyeji ndio wayajue”.

Hatimaye, alisema wenyeji wawe na mbinu ya kuhakikisha malalamishi yao yanafika kwa afisi husika “ndio sasa tuchague njia ya kuweka presha”.

“Kwa kufanya hivyo, kero yetu itashughulikiwa,” akasema.

Bi Njoroge alisema kwamba kwa sasa vile Mlima ulivyo, kuna mirengo ya Bw Kenyatta na Bw Gachagua na pia wengine ambao wameamua kuwa huru na wakisaka mustakabali wao kisiasa nje ya kudhibitiwa na hao wawili.

“Kongamano hilo la Limuru III limekosa kushirikisha watu wa Bw Gachagua na wale walio huru kimawazo huku wale wa mrengo wa Bw Kenyatta wakionekana kuwa wadhibiti wa hafla hiyo,” akasema Bi Njoroge.

Alisema kwamba “kongamano hilo litaishia tu kuwa kelele zitakazopeperushwa na vyombo vya habari, kisha tuelekee nyumbani kulala njaa huku suluhu ikiwa imetuponyoka”.

Alisema kongamano ambalo kwanza halijakusanya maoni ya wadau na ambalo hata halijafichuliwa mfadhili ni nani ni ngoma tu ya kuchafua mazingara ya kisiasa huku mtindo wa densi ukiwa hata haueleweki na unaoweza ukaishia wadau kukanyagana jukwaani.

[email protected]