Kongamano la ugatuzi kuhudhuriwa na wachache kutokana na corona

Kongamano la ugatuzi kuhudhuriwa na wachache kutokana na corona

Na WINNIE ONYANDO

KONGAMANO la ugatuzi linalotarajiwa kufanyika mwezi huu wa Agosti sasa litahudhuriwa na watu 1,000 waliochanjwa kama njia ya kupunguza msambao wa corona.

Uamuzi huo unafuatia mkutano wa mashauriano ambao ulifanyika ukiwaleta pamoja wawakilishi kutoka kwa Baraza la Magavana (CoG), Wizara ya Ugatuzi, na Wizara ya Afya.

Katika taarifa, CoG ilisema kwamba inafanya kazi na Wizara ya Afya kuhakikisha uzingatiaji mkali wa kanuni za kudhibiti corona.

“Ili kufanikisha hili, baraza la magavana kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na Kaunti ya Makueni imeanzisha chanjo kwa umma. Hivi sasa, kuna shughuli inayoendelea ya chanjo katika ofisi za CoG ili kuhakikisha kuwa wajumbe wote waliosajiliwa wamepewa chanjo kamili,” likasema baraza.

Mkutano huo utafanyika kutoka Agosti 23-26, 2021 katika Shule ya Upili ya Wavulana ya Makueni – Makueni Boys.

Ili kuhakikisha kwamba itifaki zilizowekwa na Wizara ya Afya zinafuatwa, usajili wa watakaohudhuria utafanywa mtandaoni.

Mkutano utachukua njia ya mazungumzo kupitia majadiliano ya jopo na kufuatiwa na mazungumzo ya jumla ambayo yatakuwa na sehemu kuu na vikao 14.

You can share this post!

Waiguru awataka wakazi wa Kirinyaga wachukue tahadhari...

MAPISHI: Jinsi ya kupika katlesi tamu za samaki