Habari Mseto

Kongamano lapendekeza mtaala mpya kukabili ukosefu wa ajira

March 19th, 2019 2 min read

NA RICHARD MAOSI

Viongozi wa kidini kutoka Kaunti ya Nakuru, wameomba serikali kusawazisha mtaala wa elimu ili kuimarisha utangamano miongoni mwa vijana, ambao wamepoteza matumaini katika swla la kupata ajira.

Wakizungumza katika hafla iliyoandaliwa katika ukumbi wa Kenya Redcross mjini Nakuru, walipendekeza mfumo wa elimu uangaziwe upya ili kuwafaidi wenye vipaji vya sanaa.

Kikao hicho kiliwaleta pamoja viongozi mbalimbali wa kaunti akiwemo, Erustus Mbui (Kamishna mpya wa Kaunti ya Nakuru), William Maiyo katibu wa kamati ya usalama na Joseph Koini ambaye ni DCIO.

Kulingana na msemaji wa dhehebu la Kiislamu la Nasoro Hamisi, pana haja ya kuhusisha jamii katika utekelezaji wa mapendekezo muhimu yanayohusu dini.

Alipendekeza kubuniwa somo maalum, litakalosaidia kuwaleta pamoja vijana kutoka kwenye madhehebu mbalimbali, ili kuzima itakadi kali inayochochea uhasama wa mara kwa mara.

“Hakuna silabasi ya kujumuisha dini ya Kikristo na ile ya Kiislamu, tunaomba mfumo mpya wa elimu uzingatie hili,” alisema.

Hili linajiri siku chache tu baada ya magenge ya kihalifu kuzuka upya katika mitaa ya Shabaab, Kenlands na Pondamali, na kuhangaisha raia hasa nyakati za usiku wakitoka kazini.

Na kwa sababu hiyo kuchochea chuki ya kidini miongoni mwa vijana wa kizazi kipya, wanaonyosheana kidole cha lawama na kulaumiana kwa misingi ya dini.

Erustus Mbui kamishna mpya wa kaunti ya Nakuru, aliyehudhuria mkutano huo alipendekeza kubuniwa kikao cha pamoja kitakachojadiliana mkondo wa kufuata.

Alihimiza kuwa hilo litawezekana endapo viongozi wa kidini, pamoja na wakazi wayea nia watashirikiana.

“Hii itatoa fursa ya kufanikisha utangamano wa kudumu miongoni mwa wakazi kwa sababu swala hili ni zito, na halifai kuchukuliwa kama mzaha,” alisema.

Mjadala wa NIBS

Mabishano makali yalizuka,kati ya wahubiri na viongozi wa kaunti,pale wakazi walipotaka kufafanuliwa kuhusu mfumo mpya wa taarifa wa NIBS kuhifadhi data.

Baadhi ya watu walionyesha wasiwasi wao wakisema serikali ilikuwa na njama ya kuruhusu nambari ya 666 ingie nchini.

Viongozi wa kidini waliteta wakisema mfumo huo upigwe marufuku kwa kuleta tumbojoto kwa wakazi .

“Serikali inasingizia kuturahisishia mambo kumbe inajaribu kutuingiza jahonamu,” mmoja wao alisema.

Kulingana na naibu kamishana wa kaunti ya Nakuru Magharibi Herman Shambi,alisema,hiyo ilikuwa ni njia mojawapo ya kukabiliana na stakabadhi ghushi.

Awali ilikuwa imesemekana chembechembe za DNA zingechukuliwa,lakini kamishna Mbui alipuzilia mbali madai hayo akisema huo ulikuwa ni uongo mtupu.

Wakazi walishauriwa kushirikiana na polisi,ili kupiga vita maovu yaliyokuwa yamekidhiri kwenye mitaa ya mabanda yanayozunguka Nakuru.

Ongezeko la idadi ya vilabu, PS (Play Station) na sehemu za burudani eneo la Shabaab likiangaziwa.

Wengi wa wafanyibiashara walikuwa wamepatiwa vibali na serikali kuendesha shughuli zao kwa mfano utakuta ghorofa moja ina vilabu zaidi ya kumi.

Shambi alishauri umma wasiogope kutoa habari muhimu kwa polisi kwa sababu wangehakikishiwa usalama wao.

Kamishna wa Kaunti ya Nakuru Erustus Mbui akiwahutubia viongozi wa kidini kwenye hafla iliyofanyika mjini Nakuru. Picha/ Richard Maosi

Eneo la Section 58 viungani mwa mji wa Nakuru, lilimulikwa tena, likiongoza kwa idadi ya sehemu za starehe kwa vijana.

Shambi alieleza kuwa vita vya pombe na mihadarati vilikuwa vimeanza kushika kasi, na misako katika mitaa mbalimbali ilikuwa ikiendelea.

Vinara wa dini waliombwa kusikiliza mapendekezo kutoka kwa umma, na kutoa suluhu kwa baadhi ya matatizo.

“Viongozi wakubaliane na kutengeneza kamati moja ya kushauriana, katika juhudi za kupigana na uhalifu,” Abdisalan Mohammed kiongozi wa kidini alishauri.

Nafasi sita za wawakilishi kutoka madhehebu ya Kiislamu, Kikristo na Kihindu zitabuniwa,katika kipindi cha wiki mbili zijazo,katika juhudi za kukabiliana na wahalifu.