HabariSiasa

Kongamno la Ugatuzi: Uhuru ahutubia wajumbe kidijitali

April 24th, 2018 1 min read

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta Jumanne alikosa kufika katika kongamano la tano wa Ugatuzi ulioandaliwa mjini Kakamega.

Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru aliujulisha mkutano huo kuwa Rais Kenyatta ambaye alitarajiwa kuufungua rasmi, angeuhutubia kimtandao kutoka Ikulu ya Nairobi.

Kitengo cha Habari za Rais (PSCU) kilithibitisha kuwa Rais hangefika kama ilivyokuwa imetarajiwa.

“Rais Uhuru Kenyatta atahutubia wajumbe katika kongamanno la tano wa Ugatuzi unaondaliwa katika kaunti ya Kakamega, kwa televisheni kutoka Ikulu ya Nairobi,” PSCU ikasema kwenye ujumbe katika ukurasa wake wa Twitter.

Duru ziliambia “Taifa Leo” kwamba safari ya Rais Kenyatta kwenda Kakamega kwa ndege, ilikatizwa dakika za mwisho kutoka na hali mbaya ya anga.

Mvua nyingi ilishuhudiwa jijini Nairobi, na maeneo yaliyo karibu Jumanne asubuhi, hali ambayo ilitatiza usafiri wa barabarani.

Hata hivyo, haijulikani ni jinsi gani mvua ilitatiza safari ya Rais Kenyatta.

Katika Shule ya Upili ya Kakamega, mahala pa mkutano, usalama ulikuwa umeimarisha na wakuu wote wa usalama eneo hilo walikuwa wakimsubiri Rais Kenyatta.

Hata hivyo, baada ya dakika chache Gavana Waiguru alitangaza katika hotuba yake kwamba,”rais ataungana nasi kupitia video ya intaneti”.

Hii ilikuwa dakika chache baada ya mwenyeji wa mkutano huo Gavana Wycliffe Oparanya kuelezea matumaini kuwa Rais kufika kama ilivyoratibiwa.

Hatimaye Rais alitubia mkutano kupitia mtandao wa linki ya video, mara ya kwanza kwake kuhutubu kwa njia hiyo ya kiteknolojia tangu mikutano ya ugatuzi kuanza mnamo 2014.

Hatua ya Rais kuhutubia mkutano huo kwa njia hiyo ni ishara kwamba hatimaye serikali imeamua kukumbatia teknolojia na mifumo ya kidijitali wakati maafisa hawawezi kufika mahala pa mkutano.