Habari Mseto

Konokono nao wavamia mashamba ya Mwea na kuharibu mpunga

March 26th, 2020 1 min read

Na GEORGE MUNENE

KONOKONO wamevamia mradi mkubwa wa kunyunyizia mashamba maji wa Mwea Irrigation Scheme na kusababisha uharibifu mkubwa katika mashamba ya mchele.

Wakulima wanahofia kwamba wadudu hao wataharibu kabisa mimea ambayo walipanda majuzi.Maeneo yaliyoathiriwa zaidi ni Kimbimbi, Mathangauta, Thiba, Kiorugari, Murubara na Nguka ambako mchele hukuzwa kwa wingi.

Mradi wa Mwea ni wa ekari 30,350 ambapo ekari 22,000 zinakuzwa mchele huku zilizosalia zikitumiwa kwa makao na kilimo cha mimea mingine ya chakula.

Kulingana na wakulima, konokono hao wanakula mimea yao na kuwasababishia hasara kubwa. Mwea ndilo eneo linalokuza mchele kwa wingi nchini na wakulima wanahofia kuwa huenda wadudu hao wakaharibu mimea yao yote ikiwa hatua za kuwaangamiza hazitachukuliwa.

Mkulima Alfred Miano alisema konokono hao waliharibu mimea aliyokuwa amepanda eneo la Kimbimbi. Nilizamika kupanda upya baada ya mimea yangu ya mchele kutafunwa na konokono hao,” alieleza.

Wakulima hao wanaomba serikali ya Kaunti ya Kirinyaga kuwasaidia kuangamiza wadudu hao kwa sababu kilimo kimegatuliwa.

Walisema wanategemea mchele kulisha na kusomesha watoto wao na hivyo basi serikali inafaa kuchukua hatua za haraka kuwatafutia suluhu ya tatizo la konokono hao.

“Hii ni mara ya kwanza konokono kuvamia mradi huu. Hatukuwa tunajua wanaweza kutafuna mimea,” alisema mkulima mmoja.

Wakulima hao wanasema kuna uhaba wa mchele nchini kwa wakati huu na hali inaweza kuwa mbaya zaidi, konokono hao wakiendelea kuharibu mimea yao.

Mradi wa Mwea hutoa asilimia 80 ya mchele wote unaokuzwa nchini. Mtaalamu wa Kilimo Paul Kiige alikiri kwamba konokono hao wanaweza kusababisha hasara kubwa wasipoangamizwa.