Habari

Konstebo apatikana amefariki katika hali ya kutatanisha kwake mjini Eldoret

September 12th, 2019 2 min read

Na WYCLIFF KIPSANG na MARY WANGARI

TAHARUKI imetanda mjini Eldoret, Kaunti ya Uasin Gishu, baada ya konstebo kupatikana akiwa amefariki katika nyumba yake, huku maswali yakiibuka kuhusu usalama wa maafisa wa polisi nje ya kambi zao.

Majirani waligundua mwili wa Bi Robina Moraa uliokuwa umelala katika kidimbwi cha damu nyumbani mwake eneo la Miti Moja, viungani mwa mji wa Eldoret, huku wimbi la ukosefu wa usalama likizidi eneo hilo.

Mwili huo ulikuwa na majeraha kadha ya kudungwa.

Maafisa wenzake waliowasili katika makao hayo walibubujikwa na machozi baada ya kuutazama mwili wake huku wengine wakizingira eneo la tukio kuzuia umma uliokuwa ukitaka kuingia nyumba hiyo.

Kulingana na anayetunza nyumba hizo, Bw Stanley Some, marehemu aliwasili nyumbani mapema Jumatano kabla ya mwanamume kijana kuwasili kwa gari.

“Mwanamme huyo amekuja hapa mara moja au mbili na sikuwa na hofu. Nilikutana naye kwenye lango alipokuwa akitoka lakini alionekana kutatizika kiasi,” akasema Bw Some.

Alisema alijulishwa Jumatano saa kumi na nusu alfajiri na wanaume wawili waliowasili nyumbani kwa afisa huyo kwamba alikuwa ameuawa ambapo alimfahamisha mzee wa kijiji aliyewajulisha polisi.

Afisa huyo alikuwa amehamia eneo hilo karibu miezi miwili iliyopita.

Mtulivu

Mwendazake alielezwa kama afisa mtulivu na mchangamfu ambaye daima alitangamana wazi na majirani.

Mkuu wa Polisi Uasin Gishu Johnston Ipara aliyezuru eneo hilo na kundi la wapelelezi alisema uchunguzi umeanzishwa kubaini waliohusika na mauaji hayo ya kinyama ya afisa huyo aliyekuwa konstebo wa polisi katika Kituo cha Polisi cha Naiberi.

“Tuna vidokezo kadha vya kuwatia mbaroni waliohusika na kitendo hicho cha kikatili. Hatuna hofu kuhusu maafisa wanaoishi nje ya kambi maadamu hiki ni kisa cha kipekee. Kaunti ni salama, wahalifu wachache tu wanasababisha balaa na tutakabiliana nao vilivyo,” akasema Ipara.

Serikali iliidhinisha hatua ya maafisa wa polisi kuishi nje ya kambi kama sehemu ya mageuzi na mpango wa mabadiliko katika kikosi hicho kuanzia Septemba13, 2018, lakini maswali yameibuka kuhusu usalama wa maafisa hao.

Kulingana na mpangilio mpya, maafisa hawatakuwa tena wakiishi katika nyumba za serikali, nyumba za mikataba ya muda mrefu, kambi au laini za polisi, lakini wataingia kwenye mikataba ya upangishaji wa kibinafsi katika maeneo waliochagua wao binafsi.