Habari Mseto

Konstebo jela maisha kwa kumbaka mwanamke aliyefika kituoni kupiga ripoti

July 3rd, 2020 2 min read

Na KALUME KAZUNGU

AFISA wa polisi aliyeshtakiwa kwa kumbaka mwanamke aliyefika katika kituo cha polisi cha Lamu kutafuta usaidizi miezi minane iliyopita amehukumiwa kifungo cha jela maisha.

Konstebo Rodgers Ouma, 32, alishtakiwa kwa kutekeleza kosa hilo katika chumba chake kilichoko katika makazi ya polisi mtaa wa Langoni mjini Lamu mnamo Desemba 8, 2019.

Mahakama ilikuwa imeelezwa kwamba mwanamke huyo alikuwa amefika kituoni saa mbili usiku kupiga ripoti kwamba mumewe alikuwa akimlazimisha kuavya mimba.

Muda mfupi baada ya mwanamke huyo kuondoka kituoni, mshukiwa alimfuata ambapo alimsimamisha na kumwahidi kwamba angemsaidia kupata haki katika kesi dhidi ya mumewe.

Wakati wa mazungumzo hayo, mvua ilianza kunyesha, ambapo Ouma alimuomba mlalamishi waingie katika chumba chake.

Baada ya kuingia chumbani, Ouma alifunga mlango kwa ndani na kisha kumpokonya simu mlalamishi na kuizima.

Mahakama iliambiwa alimbaka mwanamke huyo kwa muda wa saa moja kabla ya mlalamishi kupata mwanya baadaye na kutorokea nyumba ya jirani yake kwani funguo za nyumba yake pamoja na handibegi alilazimika kuziacha kwenye chumba cha polisi huyo.

Siku iliyofuata, mlalamishi aliripoti yaliyotokea na hivyo konstebo huyo akakamatwa na kufunguliwa mashtaka.

Jumatano, mahakama ya Lamu ilimpata na hatia ya ubakaji na kosa lingine la kutumia vibaya cheo chake kama afisa wa polisi na kumdhulumu raia.

Mahakama kupitia Hakimu Mkuu wa Lamu, Allan Temba ilitenga Ijumaa kuwa siku ya kutolewa kwa hukumu ya afisa huyo wa polisi.

Akitoa hukumu hiyo, Bw Temba alisema mshtakiwa hakuonyesha korti yoyote kwamba alijutia kitendo chake na badala yake amekuwa akimtishia maisha mlalamishi kwamba angemuua endapo ataachiliwa kutoka gerezani.

Bw Temba alisema mahakama pia ilipokea ripoti kutoka kwa mlalamishi kwamba tayari amekuwa akifuatwa na watu fulani, ikiwemo maafisa wengine wa polisi anaoshuku huenda wanataka kumwangamiza kupitia ushauri wa Bw Ouma.

“Kufuatia kitendo cha mshukiwa kutoonyesha kujutia kokote kwa kosa lake, mahakama imemhukumu kifungo cha maisha gerezani katika kosa lake la kwanza la ubakaji. Pia atahudumia kifungo kingine cha miaka kumi katika kosa lake la pili la kutumia vibaya cheo chake cha afisa wa polisi. Mhukumiwa yuko na siku 14 za kukata rufaa kuhusiana na hukumu hiyo,” akasema Bw Temba.

Wakati huo huo, korti imeamuru mlalamishi afidiwe Sh400,000 kama kifuta machozi kwa madhila aliyopitia ya kuingiliwa bila ruhusa yake na hata kuumizwa sehemu zake nyeti.