Koome aagiza kesi za miaka minne zimalizwe

Koome aagiza kesi za miaka minne zimalizwe

Na RICHARD MUNGUTI

JAJI mkuu Martha Koome amewaagiza mahakimu wote kote nchini wasikize na kuamua haraka kesi zote zilizowasilishwa mahakamani miaka minne iliyopita.

Katika mwongozo aliotoa wiki iliyopita, Jaji Koome alisema mrundiko wa kesi mahakamani umekuwa kero kubwa.

“Jaji Koome ametuagiza tusikize na kuamua kwa upesi kesi zote zilizowasilishwa korti miaka minne iliyopita kwa lengo la kupunguza mrundiko wa kesi mahakamani,” Hakimu Mkuu Bw Felix Kombo alisema alipotenga Oktoba 26, 2021 siku ya kusikizwa kesi ya ughushi wa vyeti vya elimu dhidi ya Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi.

Bw Kombo alimweleza Bw Sudi kuwa Jaji Koome ameagiza kila hakimu akamilishe kesi zote zilizo na umri wa miaka minne tangu ziwasilishwe kortini.

Bw Kombo alisema yuko na jukumu la kukamilisha kesi zote zilizo na umri huo miongoni mwazo hiyo inayomkabili Bw Sudi.Bw Sudi anayewakilishwa na wakili Thomas Ruto aliomba kesi iahirishwe kwa vile wakili wake alikuwa mgonjwa.

Bw Kombo alikubalia ombi la Bw Sudi akisema, “Bw Ruto amekuwa akihudhuria vikao vyote katika kesi hiyo inayomkabili Bw Sudi ambaye ni mwandani wa karibu wa Naibu wa Rais Dkt William Ruto.”

Hata hivyo, Bw Kombo alimweleza Bw Sudi kesi inayomkabili itaendelea kwa siku tano mfululizo bila kuahirishwa kuanzia Oktoba 26, 27, 28 na Novemba 16 na 17 2021.

Hakimu alimweleza Bw Sudi kwamba kesi itaendelea awe na wakili ama bila. Bw Sudi anayehudumu kwa kipindi cha pili katika bunge la 12 amekanusha mashtaka tisa ya kughushi vyeti vya masomo alivyokabidhi tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC ndipo aidhinishwe kuwania kiti hicho cha Ubunge uchaguzi mkuu wa 2013.

Ameshtakiwa kughushi cheti cha kidato cha nne KCSE mnamo Januari 31 2013 akidai ni halali kilichotolewa na baraza la mitihani nchini KNEC.

Shtaka lingine lasema Bw Sudi alighushi cheti cha kuhitimu kutoka shule ya Upili ya Highway Nairobi.Pia amekabiliwa na shtaka la kughushi cheti cha Diploma kutoka chuo cha usimamizi wa masuala ya biashara kutoka taasisi ya usimamizi ya KIM.

Shtaka linasema alijitengenezea vyeti hivi mahala kusikojulikana nchini Kenya.Mwanasiasa huyo pia ameshtakiwa kumkabidhi afisa wa tume ya kupambana na ufisadi nchini EACC Bw Derrick Kaisha vyeti hivyo vya KCSE na Diploma ya KIM katika hoteli ya Heron Court jijini Nairobi akidai vilikuwa halali.

Bw Sudi pia anakabiliwa na shtaka la kukaidi sheria za maadili kwa kumkabidhi Bw Bernard Mutali, afisa wa IEBC vyeti hivyo katika kaunti ya Uasin Gishu.Bw Sudi yuko nje kwa dhamana.Alikanusha mashtaka tisa dhidi yake.

You can share this post!

DINI: Usiogope kushindwa, hiyo ni kama giza kabla ya...

Mudavadi ataka BBI kuangaliwa upya