Habari za Kitaifa

Koome ampelekea Ruto majina 20 ya majaji wapya walioteuliwa na JSC

May 5th, 2024 1 min read

NA RICHARD MUNGUTI

MANAIBU wawili wakurugenzi wa mashtaka ya umma (DDPP) Alexander Muteti na Tabitha Ouya ni miongoni mwa majaji 20 wateule ambao majina yao yamepelekwa kwa Rais William Ruto kupata idhinisho na kuapishwa.

Jaji Mkuu Martha Koome aliwasilisha kwa Ofisi ya Rais majina ya mahakimu 10 na mawakili walioteuliwa na Tume ya Idara ya Mahakama (JSC) kuwa majaji.

Baadhi ya mahakimu walioteuliwa kuwa majaji ni pamoja na Francis Andayi na Bi Emily Ominde ambaye amekuwa Kamishna wa JSC kwa muda mrefu.

JSC iliwahoji mawakili na mahakimu 95 waliofika mbele yake kuomba kazi ya Ujaji.

JSC imepewa mamlaka chini ya Kifungu nambari 172 (1)(a) kuwahoji na kuwateua majaji wanaohitimu kuhudumu katika wadhifa huo.

Baada ya kuwateu JSC kupitia kwa Jaji Mkuu hupeleka majina yao waliofaulu kwa Rais kuwaapisha.

JSC ilitangaza nafasi 20 mnamo Oktoba 13, 2023.

Tume hiyo ilipokea maombi 305 na baada ya kuyachuja ikateua watu 95 iliyowahoji.

Kati ya hawa 95 iliwateua watu 20 na kuacha 75.

“JSC ilifanya mahojiano kati ya Aprili 3 na Mei 3, 2024, ya watu 95 iliyowaorodhesha. Wanne walijiondoa na mmoja akateuliwa kuwa Msajili Mkuu wa Idara ya Mahakama,” Jaji Koome alisema katika taarifa aliyotoa kwa wanahabari.

Jaji Koome alipeleka majina ya majaji hao wateule 20 kuteuliwa na kuapishwa na Rais Ruto kwa mujibu wa Kifungu nambari 166(1) cha Katiba kuwa majaji.

Bw Muteti na Bi Ouyo ni viongozi wa mashtaka wenye tajriba ya juu katika uendelezaji wa kesi za umma.

Bw Muteti alikuwa anaongoza kesi ya wizi wa zaidi ya Sh63 bilioni dhidi ya aliyekuwa Waziri wa Fedha Henry Rotich.

Mahakimu wengine walioteuliwa ni John Tamar, Andrew Mwamuye, Wendy Micheni, Julius Ng’arng’ar, Stephen Nzisi Mbungi na Linus Kassan.

JSC iliwatakia ufanisi wote walioteuliwa katika nyadhifa zao mpya.