Koome atuliza hofu ya Ruto kuhusu 2022

Koome atuliza hofu ya Ruto kuhusu 2022

Na MARY WANGARI

JAJI Mkuu Martha Koome amepuuzilia mbali shinikizo za Naibu wa Rais William Ruto pamoja na wandani wake kumtaka ajiondoe kwenye kamati inayohusika na maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa 2022.

Bi Koome ni mwachama wa kamati maalumu inayojumuisha mashirika mbalimbali ya kiserikali kuhusu maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, 2022.Lakini viongozi wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) wanadai Jaji Mkuu Koome anakiuka Katiba kwa kujihusisha katika masuala ya uchaguzi.

Jaji Mkuu aliyeonekana kumkosoa Dkt Ruto na wandani wake, alishikilia kuwa hajavunja sheria kwa kushirikiana na taasisi nyingine za serikali kujadili na kupanga masuala ya kitaifa.Alisema Idara ya Mahakama haiwezi kutekeleza majukumu kivyake bila kushirikiana na asasi nyinginezo za serikali.

Akihutubia wajumbe jana katika Kongamano la Ugatuzi linalomalizika leo katika Kaunti ya Makueni, Jaji Mkuu Koome alisisitiza kuwa uhuru wa Idara ya Mahakama ni thabiti na hauwezi kutikiswa kutokana na hatua yake ya kutangamana na taasisi nyingine za serikali.

Alisema kamati hiyo ya maandalizi ya uchaguzi, haijumuishi wanasiasa ambao wanaweza kuhujumu uhuru wa Idara ya Mahakama.“Nilikutana na Kamati inayojumuisha taasisi mbalimbali za serikali kuhusu maandalizi ya uchaguzi na nikashambuliwa kwa kuandaa mkutano huo.

Tunapaswa kuelewa kuwa Idara ya Mahakama haiwezi ikatekeleza haki kwa kujitenga.“Nashangaa wanaweza kusema nini iwapo ningekutana na wanasiasa,” alisema.Jaji Mkuu huyo alisisitiza kuwa nafasi yake katika Kamati Andalizi kuhusu Uchaguzi Mkuu ujao, haiathiri kwa vyovyote kesi za kupinga matokeo ambazo zitawasilishwa kortini baada ya Uchaguzi Mkuu ujao.

Jaji Mkuu alijitetea siku moja baada ya kambi ya Dkt Ruto kulalamika kupitia mikutano ya kisiasa na kumwandikia barua rasmi ya malalamishi..Kupitia barua iliyoandikwa na Katibu Mkuu wa UDA, Veronica Maina, kwa Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati, kambi ya Naibu Rais inasema uwepo wa Jaji Koome katika kamati hiyo kunahujumu uhuru wa Idara ya Mahakama.

UDA inasema itakuwa vigumu kwa Mahakama ya Juu inayoongozwa na Jaji Mkuu Koome, kutupilia mbali matokeo ya urais iwapo matokeo yatapingwa.“Hivyo basi, nafasi yake kama mwanachama wa Kamati inayojumuisha wawakilishi kutoka IEBC, afisi ya Mwanasheria Mkuu, Wizara za Usalama wa Nchi, Fedha na ICT inatishia kuwepo kwa uchaguzi huru na wa haki,” akasema Bi Maina.

Kulingana na UDA, hatua ya Bi Koome kuhusika katika Kamati hiyo haina msingi kisheria wakiitaja kama “iliyo kinyume na katiba, haramu na inayokiuka wazi sheria.”Wanahoji kuwa, kushirikishwa kwa Jaji Mkuu katika mipangilio ya uchaguzi kutaondoa hali ya kuwepo chaguzi huru na za haki kwa sababu amebuni taswira ya kuegemea upande mmoja.

You can share this post!

Simbas yakamilisha ziara ya Afrika Kusini kwa kishindo...

TAHARIRI: Kazi Mtaani iboreshwe na iwe na uwazi

T L