Korongo Ziwa Bogoria wazidi kuangamia

Korongo Ziwa Bogoria wazidi kuangamia

NA RICHARD MAOSI

Taswira nzuri ya korongo wanaobarizi kila siku kando kando ya ziwa Bogoria , kaunti ya Baringo, imepata pigo, kutokana na idadi kubwa ya korongo wanaozidi kuangamia.

Mbali na kuwa kivutio kikubwa cha utalii katika Bonde la ufa, safari za korongo katika maziwa makuu ya Nakuru, Baringo na Bogoria zina mchango mkubwa katika sekta ya utalii.

Safari yetu katika ziwa Bogoria viungani mwa kaunti ya Baringo Taifa Leo Dijitali ilikumbana na idadi kubwa ya korongo(flamingo) wakiendelea kubarizi ufuoni mwa ziwa.

Baadhi ya korongo wanajiandaa kupaa tunapowakaribia, huku wengine wakilemewa na mwendo, kutokana na maumivu yanayosababishwa na miiba aina ya mathenge.

Ndege hawa wametamalaki sehemu kubwa ambayo sasa ni makazi ya watu, hili linajiri tangu kiwango cha maji kupanda katika ziwa Bogoria na kuwasukuma korongo vijijini kwa watu..

Hata hivyo cha kushtua ni jinsi ndege hawa wamekuwa wakiangamia baada ya kukwama kwa miti aina ya prosopis juliflora au mathenge, mmea ambao umekuwa kero kwa wakazi.

Licha ya kujaa miiba korongo wengi wamekwama baina ya mashina ya miti hii kila wanaposombwa na mawimbi ya maji au kuanguka juu ya miti wanapojaribu kupaa.

Alex Kiprono ambaye ambaye ni mfugaji wa ng’ombe anasema mimea ya mathenge ina miiba yenye sumu hatari kwa mifugo na binadamu.

Amekuwa akizuru fuo za ziwa Bogoria kutafutia mifugo wake nyasi, akidai kuwa sehemu hii ina chemichemi na vyanzo vya maji vyenye lishe ya kutosha.

Anasema kuwa siku moja aliwahi kukanyaga mwiba wa mathenge bila kujua yapata miaka miwili iliyopita, na alifikiria angepata nafuu haraka.

Alieleza kuwa sio yeye tu, kwani baadhi ya wakazi hapa walikuwa wamekatwa miguu majeraha kutokana na miiba ya mathenge yalipokataa kupona na kusababisha vidonda.

“Inisikitisha kuona idadi kubwa ya korongo wakiangamia kila siku, wanapojaribu kutua au kupaa katika ufuo wa ziwa Bogoria,”akasema.

Kiprono anasema jeraha linalosababishwa na mti wa mathenge aghalabu huchukua muda mrefu kutibika, ikizingatiwa kuwa wakazi wengi hapa hutumia miti ya kiasili kujitibu.

Idadi ya Mathenge inazidi kukaribia ziwa Bogoria, kutokana na kiwango cha maji kupanda sio tu katika ziwa Bogoria , bali pia katika ziwa Nakuru na Baringo.

Mmea huu ambao ulipandwa katika eneo la Bogoria miaka ya themanini ililenga kuongeza miti katika eneo ambalo awali lilikuwa limeanza kugeuka jangwa, vilevile kuwasaidia wakazi kupata kuni na makaa.

Ni mmea ambao unaweza kufanya vyema katika maeneo kame, na madhara yake yalianza kuonekana 1997 kutokana na mvua nyinzi ya elnino.

You can share this post!

Mechi za Kundi B NWRL zawaka moto

Didmus Barasa asema amegura siasa za wilbaro kuunganisha...