Habari Mseto

Korti kuamua iwapo itaruhusu mtoto afuate babake Amerika au asalie Kenya na nyanyake

April 30th, 2024 2 min read

SAM KIPLAGAT NA LABAAN SHABAAN

HATIMA ya uhamisho wa mtoto kutoka Kenya na kwenda Amerika iko mikononi mwa jaji Jumanne, Aprili 30, 2024.

Mahakama Kuu itaamua kama mtoto ambaye babake ni raia wa Amerika na mkazi wa Jiji la New York atakaa na nyanyake Kenya ama ataondoka.

Jaji Hillary Chemitei atasubiriwa kubamiza nyundo mezani kama mtoto huyo wa umri wa miaka minne na nusu atakaa Nairobi.

Hii ni baada ya nyanya yake kukata rufaa kwamba maslahi ya mwana huyo yatatunzwa vyema nchini Kenya.

Mapema mwezi huu, korti iliamuru mtoto huyo arejeshwe Amerika ambapo wazazi wake wangepigania utunzaji wake.

Hakimu Mkuu Mkazi Festus Terer aliamua kuwa wazazi wa mvulana huyo wako hai na nyanya yake anayetambuliwa kama MWN hana uwezo wa kuwa mlezi wake.

Kisha mahakama ikaamuru idara ya maslahi ya watoto na Inspekta Jenerali wa Polisi Japheth Koome wampeleke mtoto USA.

MWN aliteta hakimu hakuelewa malalamishi yake na kuwa alipuuza maslahi ya mtoto huyo.

Alisema kuwa babake -CAD- alimtupa mtoto na mama yake na kuwaacha jijini New York 2019 bila chakula na makao.

Anadai ilimlazimu kumchukua mtoto na amekuwa akimtunza tangu wakati huo.

Kupitia hatikiapo aliyotoa kortini, MWN alisema CAD alimwacha mtoto atunzwe na mama yake ambaye hakuwa na kazi.

Aliendelea kueleza kuwa ilibidi achukue jukumu la uzazi baada ya kudai baba alipuuza majukumu yake na kuwa binti yake hakuwa na uwezo wa kuwasaidia kwa sababu alikuwa anaendelea na elimu ya shahada ya uzamili.

Baba naye alisema kuwa yeye ni mtu mwadilifu ambaye anafanya kazi katika idara ya serikali USA.

CAD alidokeza kuwa amekuwa akimsaidia mtoto wake kwa ruhusa ya nyanya yake lakini nyanya amekuwa akimzuia kumfikia.

“Mtoto wangu amekuwa akiishi na nyanya yake kwa miaka minne na amenyimwa malezi ya mzazi yanayohitajika wakati wazazi wake wako hai na wana uwezo wa kushughulikia maslahi na mahitaji yake,” alijitetea.

MWM alikata rufaa akisema raia wa Amerika ambaye alimwacha mtoto wake nyumbani New York bila msaada wa kifedha hafai kupewa ruhusa ya kumtunza mtoto.

Aliongeza kuwa tangu Februari 2019, CAD hajawahi kuweka mpango ama kujadili mipango ya kumtunza mtoto lakini anajihisi kuwa mzazi ambaye anafaa kuishi naye Amerika.

Ushahidi uliowasilishwa kortini unasema kuwa wazazi hawa walikutana 2016 na wakaishi kwa muda kabla ya mtoto kuzaliwa.

Mama yake mtoto alihamia USA mwaka 1997 kuendeleza masomo na ameishi huko tangu wakati huo.

Mwana huyo alizaliwa Novemba 2017 eneno la Brooklyn, New York. Wazazi walikuwa wanapanga kufunga ndoa lakini wakabadili nia baadaye.